Wednesday, January 30, 2013


BIASHARA HARAMU YA WASICHANA KUTOKA TANZANIA- ZANZIBAR NA HATIMAYE UARABUNI YAZIDI KUOTA MIZIZI


Biashara ya binadamu imeibuka kwa kasi nchini na kutishia usalama wa nchi kutokana na watoto wenye umri kati ya miaka 8-15 baadhi yao wakiwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari  kusafirishwa kinyemela kwenda katika nchi za Uarabuni.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na NIPASHE kwa takribani wiki mbili, umebaini kuwa biashara hiyo imeibuka kuanzia Desemba mwaka jana na imeshika kasi Januari mwaka huu na wanaosafirishwa  wengi ni watoto wa kike kutoka mikoa mbalimbali nchini. Wapo wachache wa kiume pia.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Maji, Mboje Kanga, alipoulizwa na NIPASHE alithibitisha kupata taarifa za kuwapo kwa biashara hiyo ingawa alisema kuwa hana takwimu za watoto ambao wamekamatwa wakitaka kusafirishwa.

Tatizo la kusafirisha watoto lipo, lakini nina watu ambao wanashughulikia suala hilo pale bandarini, nitafute kesho (leo) nitakupa takwimu zote kuhusiana na biashara hiyo baada ya kuwasiliana na watu wangu.

Uchunguzi zaidi  umebaini kuwa mikoa ambayo watoto hao wananunuliwa na mawakala maalum kabla ya kusafirishwa kupelekwa nchi za Uarabuni kufanya kazi mbalimbali zikiwamo za ndani ni Mtwara, Lindi, Manyara, Pwani, Tabora, Ruvuma, Tanga na Shinyanga.

Taarifa zinaonyesha kuwa mawakala hao wakishafanikiwa kuwapata watoto hao kutoka katika mikoa hiyo huwapeleka Jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwa usafiri wa majini kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar.

Uchaunguzi umebaini kuwa watoto hao wakifikishwa Zanzibar hukutana na watu maalum ambao huwapokea na kufawanyia mipango ya kuwasafirisha kwa usafiri wa ndege au wa majini kwenda Uarabuni ambako hutumikishwa katika kazi mbalimbali.

Mawakala hao wakishafanikiwa kuwasafirisha kutoka Bandari ya Dar es Salaam, hulipwa wastani wa Dola za Marekani 5,000 (Sh. milioni 8) kwa kila mtoto wanayefanikisha kumvusha kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ili kuhalalisha safari za kuwasafirisha watoto hao, mawakala wanakula njama na baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kuandika barua zinazoelezea sababu za watoto hao kwenda Zanzibar.

Barua hizo ambazo imebainika ni za kughushi, nyingi zinaandikwa na kupigwa mihuri ya wenyeviti wa serikali za mitaa wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya barua hizo ambazo NIPASHE ilifanikiwa kuona nakala yake ianasomeka:

Tunaomba mtoto huyu asitiliwe mashaka (shaka) bali apewe ushirikiano, anasafiri kwenda Zanzibar kusalimia ndugu zake walioko huko ambao watampokea.

No comments: