Ndugu Wananchi;
Kama
ilivyo ada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema,
kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza kwa mara nyingine kwa
kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya Rais na
wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi. Siku ya leo nitazungumzia
safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia. Pia nitazungumzia ujenzi
wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya Nchi
Ndugu Wananchi;
Safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa
makubwa kwa nchi yetu. Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano wa
kirafiki baina ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi wakubwa wenye nia
thabiti ya kuja kuwekeza hapa nchini. Pia tumekubaliana kuanza
mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa ushirikiano. Mpango wetu wa
sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka 2010. Mpango ule ulitusaidia
sana kuboresha huduma za maji katika miji ya Utete mkoani Pwani na
Mpwapwa mkoani Dodoma.
Katika mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika
Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi zetu
za kuleta mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie usalama wa chakula na
kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi yetu. Aidha,
tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa kwa
programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya
upatikanaji wa umeme. Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa
kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi
za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi;
Nchini Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha African Peer Review
Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora ya Tanzania
na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla hatuna mahali
tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya. Tumepongezwa katika mambo
mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna budi
kuyaboresha. Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia kufafanua
baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa. Niliwashukuru na kuahidi
kuufanyia kazi ushauri uliotolewa. Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa
kwa kauli moja.
Vurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa Kutoka Mtwara
Ndugu wananchi;
Kama
mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya Ilala
hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la
kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam.
Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano mjini
Mtwara kupinga ujenzi wa bomba hilo. Katika maandamano yale na baadaye
kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati yakatolewa madai kuwa gesi
hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa
kufanyika Dar es Salaam yafanyike Mtwara. Pia, zilitolewa shutuma
nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa miaka mingi imewasahau na
haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa bomba hilo ni
muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na wanaharakati ni
kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka
kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutshtua sote. Baadhi ya ndugu
zetu wamepoteza maisha na mali za watu na Serikali kuharibiwa.
Ndugu Wananchi;
Katika
hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013, tarehe 31
Desemba, 2012, nililisemea jambo hili. Leo mwezi mmoja baadae, napenda
kusisitiza mambo mawili. Kwanza kwamba, si kweli kuwa Serikali inapuuza
Mikoa ya Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la kuipeleka gesi Dar
es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na gesi
iliyopo Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Serikali imefanya, inafanya na ina mipango ya kufanya mambo
mengi mazuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na
Lindi. Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na
kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda
vikubwa na vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais
Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji
maarufu kama Daraja la Mkapa. Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali
katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri ya Mikoa ya Kusini.
Serikali ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa
barabara za lami kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa
wa Ruvuma. Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia
kuimaliza. Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja hadi
Nangurukuru. Mwaka 2009 tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita 56
kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani). Ujenzi wa kilometa 36 za mwanzo
ulienda vizuri. Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho
umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya
kazi hiyo kufariki. Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata mtikisiko kiasi na
kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi tuliyoitarajia. Sasa mambo
yametengemaa na kazi inaendelea kwa kasi nzuri. Matumaini yetu ni kuwa
ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Hali
kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la
kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa
barabara ya lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Tumelikamilisha
Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka
umekamilika. Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea na kwenda
Darajani umefikia mahala pazuri. Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka
Tunduru hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa. Kama mambo yataenda
sawa miezi mitatu ijayo mjenzi atapatikana. Wakati huo huo ujenzi wa
barabara kutoka Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo – Tunduru
unaendelea. Hivyo basi, kwa barabara ya “Mtwara Corridor” kazi
iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay ambayo tutaifanya wenyewe
kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na Somanga – Ndudu na
Daraja la Umoja.
Ndugu Wananchi;
Ipo
pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili iweze
kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini, kuhudumia
na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika utafiti,
uchimbaji na uendelezaji wa gesi. Pia iweze kuhudumia shughuli za
kiuchumi zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na zilizopo sasa.
Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale Mtwara tarehe 25
Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa kuhudumia
vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na
mafuta katika pwani ya Afrika ya Bahari Kuu ya Hindi. Pia waliomba kuwa
sehemu hiyo ya bandari iwe bandari huru. Niliwakubalia bila ya kusita
na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa na kutangazwa rasmi kuwa
bandari huru. Vile vile waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa
kuendeshea shughuli na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya kuchakata
gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta na kuelezwa
mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji kupanuliwa na
kujengwa upya. Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya Bandari walikuwepo
na walinihakikishia kuwa watafanya hivyo.
Tayari
eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68. Eneo la
bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya Dangote na
makampuni ya gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa kupanua bandari iliyopo,
kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu ipo
katika hatua mbalimbali za matayarisho na utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga upya
bandari ya Lindi imefikia hatua nzuri. Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe.
Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012
nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya
tarehe 1 mpaka 5 Desemba, 2012. Hali kadhalika mipango ya kujenga
bandari ya Kilwa iko mbioni. Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya
makampuni yaliyogundua gesi baharini wameamua kujenga bandari na kituo
cha kuchakata na kusarifisha gesi nje ya mkoa huo kama ilivyo kwa
Mtwara. Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia ni kuamua
mojawapo ili ujenzi uanze.
Ndugu Wananchi;
Nilipotoka bandari ya Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha
VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA taifa na wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa mafunzo mahsusi
yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta. Nilisisitiza kwamba
tuwapatie vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya
gesi na yale yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo. Nilisema
tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje na
hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.
Nafurahi
kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo. Hivi sasa katika
chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa. Kampuni ya PetroBrass ya
Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka mkoani
Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na Kampuni ya Gesi ya
Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya Uingereza,
kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing Employerbility
Through Vocational Training. Programu hii inalenga kutoa kozi
zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa katika sekta ya gesi.
Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed
Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu Wananchi;
Chini
ya programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi wanaongezewa
ujuzi ili waweze kufikia viwango vya kimataifa. Vile vile, Wizara ya
Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa kudhamini wanafunzi 50
kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao tayari wameshahitimu
mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma viwandani. Mchakato wa kuwapata
wanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama hayo kutoka mkoa wa Lindi
unaendelea. Nimeambiwa mpaka wameshawapata vijana 25 bado 25.
Hali kadhalika, Wizara ya Nishati na Madini inadhamini wanafunzi
10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kozi za mafuta na
gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa kwa wanafunzi
wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa katika mafunzo
haya. Wamepatikana watatu. Wataalamu hawa na wengine wa fani
mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha shahada ya
kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze kwa
wataalamu wa sekta hii.
Kupanga Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa
na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara. Katika
mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango kabambe
wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao
utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa
uchumi wa gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda,
biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na
burudani, viwanja vya michezo na kadhalika. Kazi ya kutayarisha
Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Makazi.
Kwa
upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa makampuni 51 yameonyesha
nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za uchukuzi na
huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni kutengewa maeneo ya
kujenga, waanze. Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya mji wa
Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu kufanyika. Viwanda
hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na Watanzania
kwa jumla. Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa kiwanda cha saruji
watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla hata ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na
mipango ya kutumia gesi ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha
umeme, kuzalisha mbolea na kutumika katika kiwanda cha saruji. Kwa
upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuzalisha
Megawati 300 kwa kushirikiana na mwekezaji binafsi. Bahati mbaya wakati
wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji huyo akashindwa
kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa. Haukufa wala
haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama ambavyo imekuwa
inapotoshwa kwa makusudi. Mradi huo bado upo, tena mpango wa sasa ni
kujenga Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi
ya taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa
upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji wengi wameshajitokeza tangu
mwaka 2008 mpaka sasa. Mchakato umefanyika wa kuchambua wawekezaji
wenye sifa na kutambuliwa. Mambo mawili yamechelewesha utekelezaji
kuanza. Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya Artumas iliyokuwa
mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (T.P.D.C) wakati ule,
kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia gesi. Wawekezaji
walitaka bei ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya Artumas na T.P.D.C.
hawakuwa tayari kupunguza zaidi ya kiasi walichopunguza, ambacho
wawekezaji bado waliona hailipi kwa kuzalisha mbolea.
Sababu
ya pili ni matatizo ya kifedha yaliyoikumba kampuni ya Artumas katika
kipindi hicho. Kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa
uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas iliathirika na
kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine. Katika kipindi hicho
ilichopitia kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea
hayakuweza kupewa kipaumbele. Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na
T.P.D.C. ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika ujenzi wa kiwanda cha
mbolea. Serikali imekubali rai yao hiyo na wanaendelea na matayarisho.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni ya
Dangote ucheleweshaji ulikuwa kwa sababu mbili. Kwanza, kampuni ya
Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa. Hoja yao
ilikuwa kwamba eneo la ziada walilokuwa wanaliomba ndilo lenye malighafi
nyingi na bora kwa utengenezaji wa saruji. Hivyo, waliamua kusubiri
mpaka watakapopewa eneo hilo.
Bahati
mbaya eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na alikuwa na
hati miliki nalo. Halmashauri ya Mtwara iliomba Serikali eneo hilo
litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali ilikubali. Hata
hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale ulipokamilika mwenye eneo
aliupinga uamuzi wa Serikali Mahakamani. Kesi ilichukua muda
kusikilizwa na kumalizika. Bahati nzuri Serikali ikashinda na mara
baada ya uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya Dangote ikamilikishwa eneo
hilo.
Kampuni
nayo ilichukua muda kuanza. Hivi sasa, timu yake ipo kwenye eneo na
mradi uko tayari kuanza kutekelezwa. Niliambiwa kuwa katika magari
yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la mradi huu.
Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote.
Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya kweli. Ni
uzushi wa makusudi wa watu wenye nia mbaya na Serikali. Huwezi kudai
kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na kufanya
upotoshaji wa makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu.
Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba
Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana na gesi hiyo. Na, wengine
wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na kupandikiza
chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka gesi kwao.
Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo. Pili, ukweli ni kwamba
pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na
Dar es Salaam na kubaki. Gesi itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia
16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini ijayo. Hivyo
asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi na
kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na
wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka mingi
ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile vinavyohitaji
gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha. Kwa upande wa
uzalishaji umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha kuzalisha umeme
mwingi zaidi. Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha umeme wa megawati
15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala, Masasi, Nachingwea,
Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote hivi sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa
tunawathamini sana na kuwajali. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza
na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini. Aidha, sitakuwa tayari
kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya
Kusini au mkoa wo wote hapa nchini. Hiyo haitakuwa sawa. Nilishasema
siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwa kwangu mimi hakuna mkoa
ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na msimamo wangu huo ndiyo maana
tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali katika mikoa
iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya ujenzi wa barabara za
lami iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe. Mipango ya
kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya kimataifa na
uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ni ushahidi mwingine
kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu Wananchi;
Haya niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na
kuelezwa kwa kina na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika za Serikali na
Mashirika ya Umma pale Mtwara katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi
wa Serikali, dini, vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29
Januari, 2013.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa
Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kule Mtwara.
Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana kulivusha
taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi yetu tangu
Uhuru. Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Idara za
Serikali kwa mchango wao muhimu walioutoa, uliosaidia kufafanua masuala
ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri. Kwa wao nawasisitiza na
kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha jamii kuhusu shughuli wazifanyazo.
Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano haitakuwepo na wapotoshaji
hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa
Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini, viongozi wa jamii, wazee,
wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa muda waliotumia
kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake wakifafanua
masuala mbalimbali. Uvumilivu wao na uelewa wao ndivyo vilivyosaidia
kurejesha hali kuwa ya kawaida. Nawaomba nao sasa, wote kwa pamoja
washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo. Pia
watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii na kuwataka watu kuwa
waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu. Wajiepushe na maneno
au vitendo vinavyofarakanisha, kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi
ya watu au Serikali. Waambieni kuwa ghasia hukimbiza wawekezaji kwani
wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama ni ya mashaka, watatoka
kwenda kuwekeza kwingine. Vyema iwe hapa hapa nchini, lakini wanaweza
kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu Wananchi;
Nawapa pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata
kutokana na ghasia zilizofanywa. Nawapa pole waliofiwa na kujeruhiwa.
Nawapa pole waliopoteza au kuharibiwa mali zao. Kwa kweli inasikitisha
na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya kuua, kuchoma moto
nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na , kuharibu na kuiba mali
za watu. Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na haukubaliki.
Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza wajibu wao. Kwa
waliohusika iwe fundisho kwao na kwa wengineo kutokubali kutumika kwa
maslahi ya watu wengine siku zijazo. Sasa wameachwa pekee yao wakati
wenzao wako huru na kufaidi maisha
Ndugu Wananchi;
Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali pazuri. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
No comments:
Post a Comment