MANENO YA WAZIRI YANAYOTAFSIRIWA KAMA MATUSI KWA MBUNGE
Nahodha alisema mbunge huyo anapaswa kutumia akili na utafiti kabla ya kuamua kutangaza jambo lolote bungeni.
Alitoa kauli hiyo akijibu taarifa ya mbunge huyo aliyoitoa juzi bungeni, akidai kuwa askari kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda wamevuka mipaka na kuingia katika Kisiwa cha Ukerewe.
Alisema askari hao wanawapiga na kuwanyanyasa raia na hivyo kuitaka serikali itoe taarifa juu ya jambo hilo na Bunge lijadili.
Akitoa kauli ya serikali kuhusu taarifa hiyo jana, Waziri Nahodha alisema kutangaza taarifa ambazo hazijafanyiwa utafiti ni jambo la hatari, kwani zinaweza kujenga mahusiano mabaya na nchi jirani.
“Taarifa za aina hii, pia zinaweza kumtia aibu mbunge mwenyewe kwa kutangaza jambo linalopotosha umma. Moja ya sifa kubwa ya utukufu wa binadamu ni kuwa na akili, akili inamwezesha binadamu kufikiri, kufanya uchambuzi na kutathimini mambo mbalimbali,” alisema.
Bila kutaja jina la mbunge huyo, Nahodha alisema binadamu ambaye haitumii akili yake ipasavyo kutafiti na kutafakari mambo, anapoteza sifa ya kuaminiwa na watu.
“Marehemu Mao Tse Tung, aliwahi kusema kuwa, iwapo hujalifanyia utafiti jambo unalotaka kuzungumza, basi usizungumze jambo hilo,” alisema.
Kwa msingi huu, waziri huyo alisema wabunge, viongozi wanaoaminiwa sana na wananchi, wakisema ndani ya Bunge mambo ambayo hawajayafanyia utafiti wa kutosha, watapoteza heshima katika jamii.
Kuhusu taarifa za mbunge huyo, Nahodha alisema kinachofanyika wilayani Ukerewe ni operesheni ya pamoja inayofanywa na maafisa uvuvi wa serikali ya Uganda, Tanzania na Kenya ya kukamata wavuvi wanaotumia nyavu haramu na uchafuzi wa mazingira.
Alisema makubaliano hayo yanafanyika chini ya taasisi ya Lake Victoria Fisheries Organization ambapo wanachama wake sasa wanaendesha operesheni hiyo mkoani Mwanza.
Nahodha alisema operesheni hiyo inaendeshwa na maofisa uvuvi toka Kenya, Uganda na Tanzania baada ya kupata mafunzo.
Na kwamba baada ya mafunzo hayo, waliandaa kazi ya mafunzo kwa vitendo katika Wilaya ya Ukerewe kwa muda wa siku saba.
Nahodha alifafanua kwamba, kwa kuwa operesheni za namna hiyo zinachukiwa na wavuvi, Februari 4 mwaka huu, kilijitokeza kikundi cha watu waliopanga kuizuia katika Kijiji cha Buzegwa.
“Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya na hakukuwa na madhara,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Nahodha, hakuna askari kutoka nje aliyeingia Ukerewe kama alivyosema mbunge na kusisitiza kuwa, operesheni hiyo ina manufaa makubwa kwa nchi hizo tatu.
Hata hivyo, baada ya waziri kutoa taarifa hiyo, Machemli aliomba mwongozo wa spika akidai waziri amemtukana kwa kumwita hana akili.
Alisema taarifa aliyoitoa ana ushahidi nayo na alisoma orodha ya watu waliojeruhiwa kutokana na operesheni hiyo.
No comments:
Post a Comment