MNYAMA VS LIBOLO: SIMBA WASEMA KAMBI INAENDELEA VIZURI ARUSHA - WAOMBA SAPOTI
HALI
ya kambi jijini Arusha inaendelea vizuri. Kikosi hakina majeruhi mpya
na wachezaji wote wanaendelea na mazoezi vizuri. Uongozi wa Simba SC
unavishukuru sana vyombo vya habari hapa nchini ambavyo vinazidi kuarifu
jamii kuhusiana na mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Libolo ya Angola
itakayochezwa Jumapili ijayo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, uongozi wa Simba ungeomba sapoti zaidi katika namna ya kuripoti mechi hizi za kimataifa.
Kwa
mfano, leo hii kuna gazeti limeandika kuhusu umafia (unyama) ambao
Libolo wamefanyiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) la kutopewa
uwanja wa kufanyia mazoezi.
Pamoja
na maelezo mazuri ya Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, kwamba
kilichofanyika kipo ndani ya kanuni za CAF, bado gazeti hilo limeandika
kwamba huo ni unyama.
Tunaomba
kueleza machache kwa vyombo vyetu vya habari hapa nchini. Mwishoni mwa
mwaka jana, wachezaji na baadhi ya wanaounda jopo la ufundi la Timu ya
Taifa la Vijana (Ngorongoro Heroes) walipigwa na askari nchini Kongo
kwenye mechi za kuwania kufuzu michuano ya CAF kwa Vijana.
Hakuna
gazeti hata moja la Kongo lililoripoti kuhusu vipigo na mateso
waliyopata Watanzania nchini humo na timu yao ikashinda. Msimu uliopita,
Simba ilinyimwa kufanya mazoezi kwa siku tatu katika mji wa Shandi
nchini Sudan kwa sababu zisizo na kichwa wala miguu. Hakuna chombo
chochote cha Sudan kilichoripoti kuhusu tukio hilo ingawa hiyo ilikuwa
ni miongoni mwa sababu zilizosababisha Simba itolewe kwenye michuano
hiyo.
Msimu
huo huo uliopita, wachezaji wa Simba waliachwa wakipigwa na baridi ya
nyuzi joto 4C nje ya uwanja wa mazoezi kwa zaidi ya saa nzima mjini
Setif, Algeria kwenye mechi ya CAF Orange Cup... Hakuna chombo chochote
cha habari cha Algeria kilichoripoti kuhusu hili.
Hivyo ndivyo vilikuwa vitendo vya kinyama. Lakini Simba SC inaamini TFF ilifanya ilichofanya kwa mujibu wa kanuni.
Ujumbe
ambao Simba SC inataka kuufikisha kwa wadau wetu wa vyombo vya habari
ni kufahamu kwamba vyombo vyetu haviko kwa ajili ya kutetea wageni.
Vyombo hivi vinatakiwa kusaidia vilabu vya Tanzania viliwakilishe taifa
vizuri katika mashindano.
Si
nia ya Simba SC kutaka vyombo vya habari vya Tanzania vitetea unyama,
la hasha. Hata hivyo, nia ya Simba ni kuona vyombo vya habari vinakua
chachu ya kusaidia timu zetu zifanye vizuri na si kusaidia timu za
kigeni kwa vile timu zetu zikienda ugenini huwa hazisaidiwi na yeyote.
Ombi letu kubwa kwenu ni kwamba uzalendo utangulie kwenye kuripoti matukio makubwa ya kimichezo hapa kwetu.
No comments:
Post a Comment