Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed
Shein,akizungumza na Balozi Mdogo wa China aneyeishi Zanzibar,Bibi Chen
Qiman,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed
Shein,akifuatana na Balozi Mdogo wa China aneyeishi Zanzibar,Bibi Chen
Qiman,(kushoto) mara baada ya mazungumzo yao alipofika Ikulu Mjini
Zanzibar jana.Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesifu juhudi za China za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi Mdogo wa China Mhe. Bibi Chen Qiman, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika
maelezo yake Dk. Shein alimueleza Bibi Chen kuwa China imekuwa na
mashirikiano na Zanzibar kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika maeneo kadhaa ya maendeleo.
Alisema
kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria
ambao ulianzishwa na waasisi wa pande mbili hizo na kuzidi kuendelezwa
hadi hivi leo.
Dk.
Shein alieleza kuwa ujio wa Rais Xi Jinping nchini Tanzania nao umezidi
kuimarika na Zanzibar ilisaini makubaliano kadhaa na hatimae kufanya
mazungumzo na kiongozi huyo.
Dk.
Shein pia, alitumia fursa hiyo kwa kutoa pongezi na shukurani kwa
madaktari kutoka China ambao wanafanyakazi katika hospitali za Unguja na
Pemba kwani wameweza kutoa huduma nzuri na bora kwa wananchi.
Kwa
upande wa ujenzi wa hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba, Dk. Shein
alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kwa
kuimarisha huduma za afya kwa wananchi ambao wamekuwa wakisubiri kwa
hamu kubwa.
Dk.
Shein alieleza kuwa China imeweza kusaida miradi kadhaa ikiwa ni
kuipatia Zanzibar mikopo nafuu katika kuendeleza miradi ukiwemo mradi wa
maji safi na salama, ujenzi wa viwanda mbali mbali mnamo miaka ya
sabini.
Aidha,
alieleza kuwa China imeweza kuunga mkono na kusaidia sekta ya habari,
nafasi za masomo, afya, miundombinu, ujenzi wa jengo la abiria la uwanja
wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume unaoendelea, mawasiliano pamoja
na miradi mengineyo na kutumia fursa hiyo kupongeza kwa kukamilika mradi
wa mitambo ya redio huko Dole ambapo nchi hiyo imesaidia.
‘China
na Zanzibar zinahistoria kubwa za mashirikiano hivyo kuna kila sababu
ya kuyaimarisha na kuyatunza …..Pia, natumia fursa hii kutoa pongezi na
shukurani zangu kwako wewe Mhe. Chen kwa juhudi zako binafsi katika
uendelezaji wa miradi kadhaa hapa Zanzibar”,alisema Dk. Shein.
Nae
Balozi Chen alimuaahidi Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar na Tanzania kwa jumla kutokana na uhusiano na ushirikiano mwema
uliopo kati ya pande hizo.
Alisema
kuwa China inazithamini sana juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar za kuhakikisha maendeleo yanaimarika kwa kila upande na ndio
maana imekuwa ikitoa ushirikiano mwema katika kuimarisha sekta za
maendeleo na za kiuchumi.
Balozi
Chen alimueleza Dk. Shein kuwa Rais Xi Jinping amefurahishwa sana na
ziara yake nchini Tanzania hivi karibuni na kutoa shukurani kwa viongozi
na wananchi kutokana na mapokezi na makaribisho makubwa aliyoyapata
akiwa nchini Tanzania.
Alieleza
kuwa hatua hiyo imedhihirisha wazi kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar
inathamini sana uhusiano na ushirikiano kati yake na China sambamba na
juhudi za pamoja katika kuimarisha sekta za kimaendeleo.
Aidha,
Balozi Chen alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake imo katika kutekeleza
miradi mbali mbali ambayo baadhi yake inatarajiwa kukamilika na
kukabidhiwa kwa Wizara husika ukiwemo ujenzi wa skuli ya Msingi ya
Mwanakwereke pamoja na mradi wa taa za barabarani zinazotumia mwaganza
wa jua huku akiahidi kuanzwa kwa miradi mengine mbali mbali ambayo ni
mipya baada ya kusainiwa makubaliano.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment