Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani.
Padri
Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili aliuawa
kwa kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi mjini
hapa akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya Jumapili
katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.
Baada
ya mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha
maafisa wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa
mauaji hayo na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar
Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi
wa NIPASHE umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa
mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea
kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.
Kwa mujibu wa
uchunguzi huo, DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi na kukabidhiwa
juzi ikieleza sababu za ofisi yake kutofungua hati ya mashtaka hadi sasa
dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Jeshi la
Polisi limethibitisha kuipokea barua ya DPP ambayo inaeleza kuwa
ushahidi uliokusanywa katika jalada la kesi hiyo hauna mashiko na kwamba
mtuhumiwa hahusiki na mauaji hayo.
Chanzo cha
habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa DPP hajaridhishwa na
uchunguzi wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa pamoja na watuhumiwa
watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya askari polisi, Said Abdulrahman
aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar Oktoba 17, mwaka
jana.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa
Ali Mussa, alithibitisha hatua ya DPP kutupa uchunguzi wote wa jalada
la mauaji ya Padri Mushi na kuwataka waandishi wa habari kumtafuta DPP
azungumzie sababu za uamuzi wake wa kutokubaliana na uchunguzi wa
Polisi.
Hata hivyo, alisema kwamba Jeshi la Polisi
bado linaamini uchunguzi walioufanya kwa kushirikiana na FBI hauna
shaka na kwamba mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu mahakamani na
wataendelea kumshikilia.
Alisema kwamba kwa mujibu
wa sheria, Jeshi la Polisi jukumu lake ni kuchunguza kesi na ofisi ya
DPP jukumu lake ni kufungua hati ya mashtaka na kutetea kesi
mahakamani.
Hata hivyo, NIPASHE ilipofika katika
ofisi ya DPP, Katibu muhtasi wake alisema amepokea maagizo kutoka kwa
bosi wake kuwa waandishi wote wa habari wanaofuatilia suala hilo,
wamuone Kamishna wa Polisi kwa vile kazi aliyopewa ya kupitia jalada la
uchunguzi kabla ya kufungua kesi ameikamilisha.
“Kamishna
ndiye aliyeitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea hatua
iliyofikiwa pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa, sasa awaite tena
amalizie kazi yake ya kuwaeleza hatua iliyofikiwa baada ya Mkurugenzi
kurejesha jalada la mauaji,” alisema Katibu muhtasi huyo.
Katika
hatua nyingine, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai,
Yusuph Ilembo, jana alifika katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, kufuatia
ombi lililofunguliwa mahakamani na wakili anayemtetea mtuhumiwa wa
mauaji, Abdallah Juma Mohamed.
Abdallah Juma
amefungua ombi katika Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha sheria 390
cha sheria namba 7 ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004,
akitaka Jeshi la Polisi litoe maelezo kwa nini mteja wake hajafikishwa
mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa Machi 17, mwaka huu.
Wakili
Abdallah Juma akisaidiwa na mawakili Shaban Juma Bakari na Shaibu
Ibrahim Shaibu waliitaka Mahakama Kuu itoe amri ya kuachiwa kwa mteja
wao kutoka mikononi mwa Jeshi la Polisi. Hata hivyo, Ilembo alisema kuwa
kutokana na uzito wa kesi hiyo, anaomba kupewa muda wa kutayarisha
majibu ya hati ya kiapo kwa maandishi na kuuwasilisha kwa upande wa
utetezi na mbele ya mahakama hiyo kabla ya ombi hilo kuanza kusikilizwa
na kutolewa uamuzi.
“Tunaomba mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na Polisi, wakati tukifanya matayarisho ya kujibu hati ya kiapo,” alisema Ilembo.
Kwa
upande wake Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema baada
ya kusikiliza pande zote mbili, alimtaka Ilembo awe amejibu kwa
maandishi hati ya kiapo ya maombi hayo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa
shauri hilo Aprili 8, mwaka huu.
Aidha, Jaji
alisema wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, ametaka mtuhumiwa huyo
afikishwe mahakamani, baada ya hoja za upande wa mawakili wanaomtetea
kutaka dhamana kwa mteja wao, kwa vile bado hajafikishwa mahakamani kwa
tuhuma za mauaji.
Kutupwa kwa uchunguzi wa
jalada la mauaji hayo pamoja na jalada la uchunguzi wa mauaji ya Polisi
kunadhihirisha kuwapo kwa mvutano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi
Zanzibar na ofisi ya DPP.
No comments:
Post a Comment