UKATILI wa kusikitisha! Watoto watatu wa famila moja, wameuawa kikatili kwa kunyongwa huku mama yao akishuhudia. Miili yao pamoja na mama yao akiwa hai, wakatumbukizwa katika kisima cha maji. Baba wa watoto hao, Justine Albert (24) anatuhumiwa kufanya unyama huo.
Kabla ya mauaji hayo, inadaiwa baba huyo
alimfunga kamba mkewe na kumziba mdomo kwa kitambaa ili asipige kelele,
kisha akaanza kuwanyonga watoto wake wote watatu kwa zamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi,
Dhahiri Kidavashari, alisema mauaji hayo ya kikatili yalifanyika juzi
saa 11:30 alfajiri katika Kijiji cha Majimoto, Bonde la Ziwa Rukwa
wilayani Mlele mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, kisa
cha kufanya mauaji hayo ni mzozo wa mtuhumiwa na mkewe, Jacqueline
Luvika (21), kwamba baadhi ya watoto hao mama huyo kazaa na jirani yao.
Watoto hao ni Frank Justine (6), Elizabeth Justine (4) na kitinda mimba Maria Justine, mwenye umri wa miezi minne.
Baada ya kuwanyonga watoto hao, inadaiwa
baba huyo alibeba miili ya watoto Frank na Eliza, na kwenda
kuwatumbukiza kwenye kisima cha jirani yao, Kawaida Jonas.
Kwa mujibu wa
madai ya Kamanda Kidavashari, mtuhumiwa baada ya kuwatumbukiza watoto
hao kisimani, alimfungua kamba mkewe na kumtoa kitamba alichomziba
mdomoni, kisha akamburuta hadi kwenye kisima hicho na kumtumbukiza.
Kugundulika Baada ya matukio hayo
yanayodaiwa kufanyika alfajiri, kulipopambazuka baadhi ya wakazi wa
kijiji hicho, waliodamka kwenda katika shughuli zao, waliuona mwili wa
mtoto ukiwa umetelekeza kando ya njia na kutambua kuwa ni Maria, ambaye
ni kitindamimba katika familia hiyo.
Inadaiwa wakazi hao walisitisha safari
yao na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa, kumpatia taarifa hiyo ya
kuhuzunisha, huku wakiuliza mama wa mtoto aliko.
Kamanda Kidavashari
alidai mtuhumiwa aliwaeleza wakazi hao kuwa mama wa mtoto huyo, alikuwa
ametoroka kwenda kusikofahamika na watoto wote.
Majibu hayo ‘rahisi’ kwa mujibu Kamanda
Kidavashari, yalisababisha wakazi hao wamtilie shaka mtuhumiwa, wakaamua
kutoa taarifa kituo cha Polisi kijijini hapo, ambao walifika ulipo
mwili wa mtoto Maria.
Wakati wakiwa katika eneo la tukio,
Kamanda Kidavashari alidai walibaini alama za mburuzo ardhini, wakaanza
kuifuatilia na zikawafikisha kisimani. Walipofungua mfuniko wa kisima
hicho, walishtuka kuona miili wa watu watatu, ikielea kwenye maji
kisimani humo.
Askari Polisi kwa kushirikiana na wakazi
wa kijiji hicho, waliopoa miili yote, lakini watoto hao wawili tayari
walikuwa wamefariki, huku mama yao akiwa amekunywa maji mengi na
kupoteza fahamu.
Kutokana na hali hiyo, wakazi hao
walipandwa na hasira na kwenda kuvamia nyumba ya mtuhumiwa na kumkamata
ili wamchome moto. Hata hivyo, Kidavashari alisema polisi walifanikiwa
kufika kwa wakati katika eneo hilo na kumwokoa mtuhumiwa, ambaye kwa
sasa bado ameshikiliwa Polisi kwa mahojiano.
Mama wa watoto hao kwa mujibu wa Kamanda
Kidavashari, alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Kijijini cha Mamba
wilayani humo, ambako amelazwa kwa matibabu, lakini hadi jana bado
alikuwa amezirai. Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu
baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lake kukamilika.
No comments:
Post a Comment