Monday, May 27, 2013

RAIS NKURUNZIZA WA BURUNDI AJA KUHUBIRI INJILI TANZANIA



Rais Pierre Nkurunziza.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, anatarajiwa kuja nchini Agosti, kuhubiri Injili katika mkutano mkubwa wa Injili unaoandaliwa na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste nchini (PCT), imefahamika.

Kwa mujibu wa Askofu Samson Mlawi aliyezungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki, tayari  Kamati ya  Maandalizi imefanya vikao kadhaa ambavyo pamoja na mambo mengine, kamati ndogo zimeundwa ili kurahisisha ujio wa Rais huyo.


Alisema, kwa kutambua umuhimu na uzito wa ujio huo katika shughuli hiyo ya kiroho, kamati imeweka mtandao wa mawasiliano kuhakikisha waumini wa madhehebu hayo kutoka mikoa mbalimbali wanahudhuria mkutano huo ambao bado unatafutiwa uwanja.

Askofu huyo alisema Rais Nkurunziza pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kuleta ujumbe wa amani na uvumilivu wa kidini hususan katika kipindi hiki cha mpito baina ya madhehebu ya Kikristo na Waislamu nchini.
 

“Mimi na wanakamati wenzangu, tunaamini Mungu atafanya kazi yake kupitia Rais kuhubiri Habari Njema kwa Watanzania kama ambavyo angehubiri mtu mwingine yeyote, lakini kutokana na nafasi yake ni matumaini yetu kwamba ujumbe huo utachukuliwa kwa uzito wa kipekee,” alisema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Askofu, mwezi huo huo wa Agosti, Mwinjilisti wa Kimataifa wa Huduma ya Christ For All Nations (CFaN), Reinhard Bonkke anatarajiwa kuwasili nchini kwa ujumbe maalumu kwa waumini wa madhehebu ya Kikristo na  Taifa kwa ujumla.
 

Alisema, ujio wa wageni hao mashuhuri nchini, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza shaka na wasiwasi kwa baadhi ya Wakristo ambao wako njia panda kuhusu masuala muhimu ya kiimani, ikiwa ni pamoja na suala la kuchinja.
 
Source:MPEKUZI HURU

No comments: