Friday, May 3, 2013

SI KILA MSAADA UNAOPEWA ASANTE YAKE NI KUMVULIA NGUO MWANAUME


Sote tunajua katika penzi la kweli kuna kujaliana katika shida na raha na kuonyesha upendo wa mtu kwa mwenzake.

Tunajua wote katika mapenzi  kuna kupendana ili kukamilisha pea ya upendo ikimaanisha kila mmoja ampende mwenzake kwa dhati.

Penzi la upande mmoja tumeona si kamili kwa vile mpendaji huwa mmoja na mwingine huwa yupo na mwenzake kwa sababu fulani, akishakidhi haja zake huondoka bila kwa heri na kusababisha mateso kwa mmoja.


Kuna tatizo limejitokeza kwa kina dada kuamini mtu anayempa msaada basi anamhitaji kimapenzi. Kweli anayekusaidia lazima atakuwa mtu anayejua utu wa mtu bila kuangalia anakujua au la.


Sehemu hii imekuwa ikiwachanganya wengi na kuingia kichwakichwa mwisho kuachwa njia panda na kuona umegeukwa, yaani mtu uliyemuamini amekugeuka.

Kwa nini?
Upendo na msaada ni vitu viwili tofauti, msaada umo ndani ya upendo kwa maana anayekupenda atakusaidia katika shida na raha, lakini si kila msaada una upendo.

Kwa sababu gani?
Tumeona kwenye usafiri wanawake wamekuwa viumbe dhaifu pale wanapopewa msaada na mwanaume na huamini msaada ule ni dalili za kupendwa, kumbe aliyetoa msaada hakutoa kama sehemu ya kuonyesha anakuhitaji kimapenzi bali kukusaidia kama mwanadamu mwenzake.
Wanawake wengi wamekuwa wakipoteza dira ya maisha kwa kuanzisha uhusiano na mtu anayekutana naye safarini na kumpa msaada kama chakula au kumsaidia mtoto. 
Baada ya msaada huo mioyo yao huwa dhaifu na kuamini yule ndiye mwanaume sahihi kwa vile kamsaidia bila kumjua pengine msaada huo haupati kwa mwenza wake.
 
Mara moja huanzisha uhusiano na kupeana namba za simu ili watafutane baadaye. Wanawake wengi hufikia hatua ya kuzikana ndoa zao kwa vile tayari mioyo yao imeishakurupuka bila kufikiri.

Wengi wao wamekuwa wakifunga hata safari kuwafuata watu hao hata kama ni mbali bila kuijua historia ya mtu waliyekutana naye kwenye gari.

Baada ya kukutana ndipo wanapokutana na tabia tofauti na waliyoifikiria, hapo ndipo yanakuja majuto. Wapo wanaodiriki kuvunja hata uhusiano wao kwa penzi la mwanaume wa safarini na kuamini aliyekuwa naye si lolote si chochote kwa mwanaume aliyekutana naye.


Hata kama hakumfuata, hicho huwa chanzo cha nyumba kuvunjika au kuingia kwenye migogoro kwa vile  akili yao wameihamishia kwa mwanaume wasiyemjua.

Baada ya kuachwa anaangukia pua kwa vile yule mtu aliyetoa msaada haukuwa kwa lengo ya kumvuta kimapenzi.


Hivyo, inatakiwa tuwe makini sana na uamuzi wetu wa kukurupuka, si kila msaada unaopewa asante yake ni kumvulia nguo mwanaume. 

Utawavulia nguo wangapi watakaokusaidia?  Kumbuka kusaidiwa ni haki yako kama mwanadamu na si kwa ajili ya kudhalilishwa.

Uheshimu utu na mwili wako, kwa sababu heshima ya mtu huijenga mwenyewe hujengewi na mtu. Usikubali kuutoa mwili wako kama asante kwa msaada utakaopewa, asante ya mdomo inatosha.
 
Kama mtatongozana hiyo ni hiyari yenu kukubali au kukataa,  uwe muwazi ili kujiweka eneo salama kwa kuheshimiwa na si kuukana uhusiano wao kwa vile tu umenunuliwa chipsi na kuku pengine soda na kitafunwa.
 
Akitoa ni kwa upendo wake una haki ya kukubali au kukataa si kila upewacho lazima ukubali kuchukua na asante yako ni kuutoa asusa mwili wako!

No comments: