KATIKA hali isiyo ya kawaida na inayoashiria uzembe katika ulinzi wa
mbio za Mwenge wa Uhuru, juzi kijana mmoja mkazi wa eneo la Phillips
katika Kata ya Sekei jijini Arusha, Hamad Rashid (32) aliiba kiti
(kigoda) cha kukalishia Mwenge.
Kuibwa kwa kiti hicho kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas. Kiti hicho hutumika kuwekea Mwenge wa Uhuru
unapokuwa katika mbio zake nchi mzima.
Tukio la kuibwa na kisha kukamatwa kwa mtuhumiwa lilitokea juzi saa
11 jioni Sanawari eneo la Mataa. Eneo hilo ndilo lilipangwa kwa ajili ya
mkesha wa Mwenge huo baada ya kukamilisha mbio zake na kazi ya kuweka
mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji
la Arusha.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Sabas aliyetafutwa kwa njia ya simu
kuzungumzia tukio hilo, alikiri kutokea kwa wizi huo na kuongeza kuwa
mtuhumiwa huyo alishakamatwa na polisi waliokuwa wakiulinda Mwenge
pamoja na kiti hicho.
Alisema tukio hilo lilitokea wakati Mwenge huo pamoja na wakimbizaji
wake kitaifa, kimkoa na viongozi wengine wakiwa katika harakati za
kusoma salamu za utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla
ya ratiba ya utangazaji wa ratiba ya mkesha kutolewa.
Alisema kabla ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, alionekana kwa muda
mrefu akiwa amesogelea gari lililokuwa limebeba kiti hicho kilichoelezwa
na kamanda kuwa kilikuwa cha akiba.
Alisema mara baada ya wizi kijana huyo alikamatwa na katika mahojiano
alisema alikuwa anataka kukiangalia tu na kwamba haikuwa nia yake
kukiiba na kuomba msamaha.
Hata hivyo alisema polisi wanaendelea kumhoji ili kubaini dhamira
halisi ya kukichukua kiti hicho.
Alisema mara baada ya upelelezi wa kesi
hiyo, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani ili kujibu mashitaka
yanayomkabili ya wizi wa kiti hicho cha Mwenge wa Uhuru.
Mwenge huo wa Uhuru uliingia Arusha Juni 3 mwaka huu ukitokea mkoani
Manyara na utakimbizwa katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Arusha kabla
ya kukabidhiwa kwa mkoa wa Mara Juni 11, yaani Jumanne ijayo.
SOURCE:GUMZO LA JIJI
No comments:
Post a Comment