Wednesday, June 5, 2013

MAKALA: NI UPUUZI KUMSHUSHA THAMANI, KUMUACHA JUMA KASEJA - SIMBA IIGE MFANO WA YANGA KWA NSAJIGWA - MAN U NA GIGGS





KLABU ya soka ya Simba haikuweza kufanya vizuri msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kwani kutoka bingwa mtetezi iliambulia nafasi ya tatu msimu uliopita na kuiacha Yanga ikitwaa ubingwa. 
Hadi kutwaa nafasi ya tatu, Simba ilipambana vilivyo kwani Kagera Sugar nayo ilikuwa ikiwania nafasi hiyo kwa udi na uvumba. Jitihada za wachezaji na benchi la ufundi ndizo zilizoifanya Simba kutwaa nafasi ya tatu.
Usajili ukiwa unaendelea, Simba imeshamsajili kipa Andrew Ntala kutoka Kagera Sugar, huku tayari ikiwa na makipa Juma Kaseja na Abel Dhaira. Usisahau yule wa kikosi cha pili cha timu hiyo.
Wakati Simba ikilundika makipa hao, mkongwe Kaseja ni kama hatakiwi tena na timu hiyo, kwani kitendo cha kumsajili kipa namba moja wa Kagera, Ntala huku Dhaira akiwepo kikosini inaonyesha wazi mmoja kati ya Kaseja au Dhaira anatakiwa kuondoka.
Dhaira hadi anatua Simba alikuwa kipa wa kutegemewa wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, hata huyu Ntala naye ni tegemeo la Kagera. Hii ina maana wote hao sasa wanatakiwa kupambana na Kaseja kuwania nafasi ya kwanza kikosini.
Ni ngumu kwa Simba kuachana na Dhaira kwani mkataba wake ni mkubwa na ambao unaweza kuigharimu Simba kiasi kikubwa cha fedha kuuvunja.
Popote pale duniani, huwezi kusajili makipa namba moja wawili kutoka timu nyingine huku tayari ukiwa na kipa hodari. Hii ni sawa na usajili mwingine wa nafasi nyingine uwanjani.
Tayari kuna tetesi kwamba, Simba ipo tayari kumwachia Kaseja ajiunge na klabu nyingine kwa madai ya kushuka kiwango na kushindwa kuisaidia timu kushika moja kati ya nafasi mbili za juu.
Mchakato mzima wa kuhakikisha Kaseja anaondoka Simba unaongozwa na kiongozi mmoja ambaye sasa ana sauti ndani ya klabu hiyo na mbaya zaidi hakuna sababu za msingi za kumuacha Kaseja.
KUSHINDWA KUISAIDIA SIMBA
Sababu kwamba Kaseja ameshindwa kuisaidia Simba haingii akilini kutokana na ukweli kwamba hata katika mechi ambazo Simba imefungwa Kaseja akiwa langoni, kuna vitu vingi vilikuwa vinatokea.
Hadi sasa hakuna hoja ya msingi iliyotolewa na uongozi juu ya mpango huo unaotengenezwa wa kuhakikisha Kaseja anaondoka Simba kwa njia yoyote ile, bali inayolazimishwa ni hii ya kushindwa kuisaidia timu.
Hawafafanui jinsi kipa huyu alivyoshindwa kuisaidia Simba kushika moja kati ya nafasi mbili za juu, kwani hajawahi kufungwa mabao manne katika mechi moja na idadi kubwa ya kufungwa kwake katika mchezo mmoja haizidi mabao matatu.
HAKUWA NA WASAIDIZI WA MAANA
Ikumbukwe ya kwamba, Kaseja ni kipa imara anapokuwa na mabeki imara, sasa tazama ndani ya msimu huu alikuwa na mabeki wa kati wa aina ipi na walikuwa na uwezo upi.
Msimu wa 2011/12 ambao Simba ilitwaa ubingwa, kwa kiasi kikubwa Kaseja alilindwa na mabeki Juma Nyosso na Kelvin Yondani, hao aliweza kuwapanga ipasavyo na ni safu iliyokuwa ikielewana kwa muda mrefu.
Msimu uliopita Kaseja amecheza na safu nyingi za ulinzi wa kati Victor Costa, Nyosso, Shomari Kapombe, Komalbil Keita, Pascal Ochieng, Mussa Mudde hadi chipukizi Hassan Khatib. Tazama mlolongo huo wa mabeki.
Utitiri huo wa mabeki haukuweza kumsaidia Kaseja kwani ulikuwa ukibadilika kila mara na mwisho wake hata kocha Patrick Liewig akawa anafanya kazi ya kujaribu mabeki hadi ligi inaisha.
Tazama kiungo Mudde aliyesajiliwa katika timu kama kiungo lakini kutokana na uhaba wa mabeki, Simba ikaamua kumchezesha kama beki. Mbaya zaidi akachezeshwa katika nafasi hiyo kwenye mechi muhimu kama ya Simba na Yanga.
KASEJA ANAFUNDISHWA NA NANI?

Unaweza ukaona kama utani lakini ndiyo soka lilivyo, kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ wa Yanga aliichezea Simba msimu wa 2011/12, hakuwa akipata nafasi na hata alipopewa nafasi alikuwa hafanyi vizuri kama ilivyo kwa Kaseja, ili lipo wazi.
Lakini msimu uliopita, Barthez aliipa Yanga ubingwa na kutangazwa kuwa kipa bora wa ligi nzima. Sababu zipo wazi.
Akiwa Simba, Barthez alikuwa anapata mafunzo ya ugolikipa akiwa sambamba na Kaseja, lakini alipotua Yanga ndani ya muda mfupi timu hiyo ikampa kazi Razack Siwa, ambaye pia ni kocha wa makipa wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.
Siwa ni kipa wa zamani pia aliwahi kuinoa Yanga tena kwa nafasi zote mbili, kocha mkuu na kocha wa makipa, kwa kifupi huyu amesheheni katika kufundisha makipa na ameshasoma kozi kibao za kufundisha makipa.
Katika mahojiano na kituo cha runinga cha Clouds kupitia kipindi cha Sports Bar, Siwa aliwahi kusema tatizo la wakufunzi wengi wa makipa, wanafanya mambo ambayo hayatokei uwanjani na wanashindwa kumuandaa kipa kuwa jasiri uwanjani.
Anatolea mfano kwa mazoezi ya kuwarushia mipira makipa ili wadake, Siwa anasema hilo ni tatizo kwani kipa akiwa uwanjani anapigiwa mashuti na wala harushiwi mipira na wachezaji wa timu pinzani. Siwa huwapigia mashuti makali makipa wake katika mazoezi.
Huo ni mfano mdogo tu wa Siwa, lakini kuna vitu vingi ambavyo vinamfanya Barthez aonekane anafanya vizuri uwanjani, lakini bado huyu ni yuleyule na Kaseja ni yule yule.
Barthez msimu wote huu amecheza chini ya mabeki Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na wakati mwingine Athuman Idd Chuji au Mbuyu Twite. Hao wote ni wachezaji wazoefu. Hata hivyo muda mwingi walicheza Cannavaro na Yondani.
POULSEN ANAWAKOSOA
Pamoja na Simba kumuona wa nini, bado Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen anamuona Kaseja ni kipa bora na ndiyo maana anaendelea kumuita kikosini na kumtumia pia.
Poulsen siyo kwamba haoni vipaji vya makipa Mwadini Ally wa Azam FC na Barthez, kuna kitu cha ziada anachohitaji kutoka kwa Kaseja ndiyo maana anamtumia kikosini.
Kitu ambacho Poulsen amekiona kwa Kaseja ni uzoefu ambao haupo kwa Barthez au Mwadini japokuwa wote wana viwango vinavyolingana.
SIMBA HAITAKI KUWA NA GIGGS WAO?
Ukongwe ndani ya timu ya soka ni moja kati ya vitu muhimu ambavyo klabu nyingi za Ulaya na Afrika vinahitaji ili kuzifanya ziwe na maendeleo.
Kaseja ameichezea Simba kwa zaidi ya miaka 10 sasa, maana tangu ajiunge nayo mwaka 2002 akitokea Moro United ameachana nayo mwaka mmoja tu alipotimkia Yanga.
Manchester United inapohakikisha inabaki na mtu kama Ryan Giggs kikosini huwa inahitaji maendeleo kwani damu changa peke yake si rahisi kuipa mafanikio. Wakongwe ndiyo wanaotumiwa kuweka mambo sawa kati ya uongozi na klabu.
Yawezekana Simba sasa inamuona Kaseja kama kikwazo cha wao kuwamiliki na kuwatumikisha itakavyo wachezaji chipukizi tena kwa malipo hafifu, maana yawezekana wanamuona Kaseja atawafuta mchanga machoni.
HAWAONI YALIYOTOKEA KWA CASILLAS & MOURINHO  
Ni ukweli usiofichika kwamba, kipa Iker Casillas ndiye kila kitu kati ya wachezaji wa Real Madrid na hata timu ya taifa ya Hispania. Kocha Jose Mourinho muda mfupi baada ya kutua kuifundisha klabu hiyo alitaka kufuta hali hiyo kwa Casillas.
Mourinho alitaka yeye kuwa mtu muhimu katika timu kuliko Casillas, akamtengezea mazingira kipa huyo ya kuonekana hafai na kuanza kumuweka benchi bila sababu ya msingi.
Hata hivyo, Madrid ni miongoni mwa klabu zinazothamini mchango wa wakongwe kama Casillas ambao wanaweza kuisaidia timu ndani na nje ya uwanja. Ikaamua kuachana na Mourinho ili ibaki na Casillas.
Ndiyo maana Chelsea leo hii ina John Terry, Liverpool yupo Steven Gerrard, Man United wanaye Giggs, na hata Yanga wanaye Shadrack Nsajigwa. Sasa iweje Simba imtimue Kaseja?
Umefika wakati sasa siasa na chuki zisizo na maana ziondoke katika mazingira ya soka letu ili tuweze kufikia mafanikio.
NA SHAFII DAUDI

No comments: