Suala la uwepo wa rushwa ya ngono kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) limetinga bungeni.
Suala hilo Lilijitokeza jana wakati Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), alipomaliza kujieleza bungeni akiomba kura kwa wabunge wamchague awe mjumbe kwenye taasisi hiyo.
Suala hilo Lilijitokeza jana wakati Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), alipomaliza kujieleza bungeni akiomba kura kwa wabunge wamchague awe mjumbe kwenye taasisi hiyo.
Baada ya Mbunge huyo kumaliza kujieleza, alisimama Mbunge wa Viti Maalumu, Naibu Waziri wa Jinsia na Watoto, Ummy Ally Mwalimu aliyemhoji atatoa mchango gani katika kupambana na changamoto kwenye chuo hicho, ikiwamo rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia, ili kusaidia watoto wa kike wasome vizuri.
Kabla ya Mangungu kujibu swali hilo, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo (CUF), aliomba Mwongozo wa Spika kutaka muuliza swali afute kauli yake kwani ni ya udhalilishaji na inaweza kuleta matatizo.
Hata hivyo, Spika Anne Makinda aliingilia kati na kusema hakuna haja ya kufuta kauli hiyo kwa vile ndiyo hali halisi iliyopo.
Akijibu swali hilo, Mangungu alisema atasaidiana na wenzake kuhakikisha wanakomesha suala hilo.
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo (CCM) alichaguliwa kuwa mjumbe kwenye Jukwaa la Kibunge la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC-PF) katika uchaguzi uliofanyika bungeni.
Akitangaza matokeo, Spika Makinda alisema Jaffo aliibuka kidedea baada ya kupata kura 74 na kuwashinda wapinzani wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema) aliyepata kura 56 na Mbunge wa Busanda, Lorensia Bukwimba (CCM) aliyepata kura 51. Kura 182 zilipigwa na moja kuharibika.
Pia Spika Makinda alimtangaza Mangungu mshindi na kuwa mjumbe wa Baraza la Udom kwa kupata kura 137 dhidi ya 38 za mpinzani wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Pudenciana Kikwembe (CCM). Kura 177 zilipigwa na mbili kuharibika.
Upande wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) aliyeibuka mshindi ni Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni (CCM) ambaye hakuwa na mpinzani baada ya Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu (CCM) kujitoa.
Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM) aliibuka kidedea kwa ujumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Mbeya, baada ya kukosa mpinzani.
Credit; zero99
No comments:
Post a Comment