http://muleba-kwetu.blogspot.com
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ametaka vijana kusimama imara kulinda na kulijenga taifa lao.
Alisitiza maendeleo ya taifa hili, katu hayataweza kusonga mbele, kama viongozi wake wataendelea kuendeleza vitendo vya rushwa na biashara ya dawa za kulevya.
Aidha, alisema ataendelea kupiga vita tatizo la rushwa lililopo nchini, licha ya suala hilo kuonekana kuwa mwiba mchungu kwa baadhi ya watu, ambao ili kujiepusha na ‘alizoziita kelele zake’. Aliwataka kujisafisha dhidi ya vitendo hivyo.
Sumaye alitoa kauli hiyo jana katika Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam aliposhiriki mazoezi ya kujenga mwili na mamia ya vijana kutoka klabu mbalimbali za Dar es Salaam. Mazoezi hayo yaliandaliwa na Klabu ya Ukwamani iliyopo katika kitongoji cha Kawe.
Alisema vijana ndiyo hazina ya Taifa kwa ajili ya maendeleo ya baadaye. Alisema kwamba pasipokuwepo na dhamira ya dhati ya kuwajengea misingi imara ya maisha yao, ni wazi Taifa litakosa viongozi bora miaka ijayo.
Alisema ni lazima kazi ifanyike badala ya kukaa na kuwaita ‘bomu linalotaraji kulipuka’.
Alisema kumekuwa na kauli mbalimbali zinazotolewa kuhusu vijana kuwa ndiyo wanaochochea vurugu katika maeneo mengi nchini, hivyo kuwajengea taswira mbaya aliyosema kuwa si jambo la busara kwa kuwa hawajapewa nafasi katika maeneo mbalimbali ili waweze kusukuma mbele maendeleo ya Taifa hili.
“Vijana msirudi nyuma, fursa zipo nyingi endeleeni kuzitumia, pale mnapoona hakuna nafasi hiyo tumieni fursa hiyo kuwauliza viongozi walioko juu yenu, hakutakuwa na bomu linalosubiri kulipuka kama mtawekewa misingi mizuri na msikate tamaa katika hilo,” alisema Sumaye.
Kuhusu rushwa aliwataka vijana hao kuwa makini nayo kwa kuwaepuka wale wote wanaotoa fedha ili kupata uongozi na kuongeza kuwa wale watu wote wanaofanya hivyo wanakuwa na lengo lao, hivyo ni vyema wakawaepuka mapema ili kujilinda.
Alisema rushwa kwa kiasi kikubwa ndiyo inayochangia kudidimiza maendeleo ya Taifa na kwamba wanaotoa fedha wanajua ni namna gani watairudisha hapo baadaye badala ya kuwaletea maendeleo.
“Hata uchaguzi unaokuja utawaona wanajipitisha kwa kutoa fedha, khanga na vitu vingine, nawaomba mtambue kuwa anayetoa vitu hivyo jua ni wazi kuwa amejiona hatoshi katika uongozi hivyo ni vyema akaepukwa,” alisisitiza Sumaye.
No comments:
Post a Comment