Wakati Rais Jakaya Kikwete akiponda mpango wa Chadema kuanzisha kambi za mafunzo kwa ajili ya mafunzo ya ulinzi, imeelezwa kuwa Chama Cha Mapinduzi nacho kimekuwa kikiendesha mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake.
Hata hivyo alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu
kuendesha mafunzo hayo, Naibu Katibu wa CCM, Mwigulu Nchemba alisita
kuzungumza na kumtaka mwandishi aangalie ukurasa wake wa Facebook ambako
amefafanua.
Katika ukurasa huo, Mwigulu amekosoa Rasimu ya
Katiba Mpya akisema muundo wake utaleta utata wa usalama. Mwigulu
ametaja ibara ya 223(1) inayozungumzia uanzishwaji wa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania(JWTZ), litakalokuwa na mamlaka ya kusimamia
ulinzi na usalama, “Ibara ya 232(1) inasema bila kuathiri masharti ya
Katiba hii, nchi Washarika wa Muungano wanaweza kuanzisha vikosi vya
ulinzi na usalama .... katika maeneo yao.
Ametaja pia ibara ya 227(1) inayoeleza uundwaji
wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano na ibara ya 232 inayozungumzia
vikosi vya washirika kuhusika na ulinzi wa watu wao na ibara ya 233 (1)
inayozungumzia Idara ya Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano.
“Suala la usalama ni nyeti muundo huu utategemea
tu mazingira na busara ya viongozi. Vinginevyo ni rahisi vikosi vya
Muungano kupigana na vya nchi washirika kufuatia maelekezo ya viongozi
wao siku wakitokea sio wataifa,”
Akifunga kongamano la amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Dar es Salaam juzi, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM pia alikosoa kitendo cha Chadema kususia mkutano. “Sasa hawa kweli wanapenda amani yetu wakati hawapendi tuzungumze,wanataka watu wauane,wapigane,” alisema.
Mbali na Rais Kikwete,Jeshi la Polisi kupitia
msemaji wake, SSP Advera Senso limekionya Chadema kuhusu mpango huo.
“Kitendo cha chama chochote cha siasa ikiwamo Chadema kuanzisha kikundi
cha kujihami ni kinyume cha sheria za nchi na endapo watafanya hivyo
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Jeshi la Polisi nchini
limeanza uchunguzi na litachukua hatua kulingana na ushahidi
utakaopatikana.
“Jeshi la Polisi litamshughulikia mtu yeyote
atakayekwenda kinyume cha sheria bila kujali wadhifa wake,” alisema
Senso katika taarifa yake.
Hata hivyo,mtindo wa kuanzisha vikundi vya ulinzi
kwa vyama vya siasa unaonekana kuzoeleka huku vyama vikubwa vikiwa na
makundi kama vile Red Brigade ya Chadema,Green Guard ya CCM na Blue
Guard ya CUF.
No comments:
Post a Comment