Friday, July 12, 2013

JIKO LA MAFUTA LAUA WATU WANNE WA FAMILIA MOJA HUKO ILEMELA JIJINI MWANZA...!!

  • WATU wanne wa familia moja, wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi, kuteketea kwa moto alfajiri ya jana. Ajali hiyo ilitokea eneo la Lumala Mashariki wilayani Ilemela na ilitokana na jiko la mafuta, ambalo halikuzimwa baada ya wanafamilia hao kula daku usiku; matokeo yake, lililipuka alfajiri.

  • Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na pikipiki iliyokuwa na mafuta ya petroli, ambayo ilishika moto na kuungua na kuteketeza watu waliokuwa ndani pamoja na nyumba.

  • Waliokufa ndani ya nyumba hiyo, mali ya Fadhil Nuru, ni Amina Musa (75) na Mariam Musa (72) ambao ni mtu na dada yake.

  • Wengine ni Busharat Bashir (23) na Janat Abdul mwenye umri wa miezi sita, ambao ni mtu na mwanawe. Majeruhi, Dotto Twaa mwenye umri wa kati ya miaka 17 na 18, amejeruhiwa vibaya usoni, mkononi na kifuani na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando.

  • Taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu hao, zinasema Mariam alikwenda kumtembelea dada yake huyo, Amina, aliyekuwa akiishi kwa mwanawe. Busharati na mwanawe, Janat, waliokuwa wakikaa Kirumba, walikwenda nyumbani hapo eneo la Lumala, kumtembelea baba yao mdogo na kuwaona bibi zao hao, ambao pia ni marehemu.

  • Baba ambaye ni mkuu wa familia, amenusurika. Yeye alikuwa amelala nyumba ya mbele. Hawa waliokufa na huyo majeruhi, walikuwa wamelala nyumba ya nyuma,” alisema mmoja wa wanafamilia, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini. Kamanda alisema,

  • Timu ya polisi bado ipo eneo la tukio wakiendelea kufuatilia ili kujua kama kuna majeruhi wowote waliokimbizwa kwenye zahanati na vituo vya afya ili tuweze kuwatambua”.

  • Mangu alisema atatoa taarifa zaidi leo timu itakapomaliza kazi. Mangu alisema miili ya marehemu, ilihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Hata hivyo, maziko yalifanyika jana.

  • Akizungumza katika eneo la tukio, mmiliki wa nyumba hiyo, Fadhil Nuru alisema moto ulioteketeza familia yake, ulizimwa na wananchi waliojitokeza kuwasaidia.

  • Alisema walipiga simu mapema Zimamoto, lakini walichelewa kufika na kukuta tayari majirani wamezima.

  • Kama Zimamoto wangewahi kufika kusingekuwa na madhara makubwa ya kupoteza wanafamilia wengi namna hii, hata hivyo nawashukuru wananchi kwa kunisaidia,” alisema.

 

SOURCE: HABARI LEO


No comments: