Mwita Waitara
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mjini Singida jana imetupilia mbali kesi iliyokuwa
inawakabali viongozi wawili wa CHADEMA Ndugu Mwita Waitara ambaye ni
afisa sera na utafiti makao makuu na mshauri wa chama hicho Dk Kitila
Mkumbo. Katika hukumu yake aliyeiyosoma mbele ya wakili wa washtakiwa hao Tundu Lissu, hakimu wa Mahakama hiyo Masham alisema kuwa washatakiwa hawana kesi ya kujibu kwa kuwa mashahidi wa serikali walishindwa kuthibitisha aina ya matusi yaliyodaiwa kutolewa na washtakiwa.
Aidha, hakimu huyo alisema kwamba upande wa serikali walishindwa kumleta shahidi muhimu katika kesi hiyo Mwigulu Nchemba aliyedaiwa kutukanwa ili athibitishe kwamba yeye ndiye aliyetukanwa na namna ambavyo matusi hayo yamemuathiri.
"Kushindwa kwa Mwigulu Nchemba kufika mahakamani ni kuonyesha kwamba ama hajui kwamba alitukanwa au hakuona kosa lolote alilotendewa na mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa mambo ya kuhisiwa".. alisema hakimu huyo.
Washtakiwa walidaiwa kutenda kosa hilo tarehe 14 Julai mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ndago wilayani Iramba ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo kilikuwa na mkutano wa hadhara.
Kesi hiyo imekuwa ikisuasua mara nyingi kwa upande wa serikali kushindwa kuleta mashahidi mahakamani na kusababisha kesi hiyo kuahirishwa mara kwa mara, jambo ambalo lilikuwa likimkera hakimu wa kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment