Mbunge wa Mjini Mkongwe-CUF Ismail Jussa
---
Taswira ya Zanzibar kama kisiwa cha amani imechafuliwa tena jana
usiku pale watu wasiojulikana walipofanya kitendo cha kinyama na
kishenzi cha kuwamwagia tindikali (acid) wananchi wawili wa Uingereza
katika maeneo ya Shangani, jimbo la Mji Mkongwe.
Taarifa za awali nilizozipata ni kwamba vijana hao wawili wapo
Zanzibar wakiwa ni sehemu ya vijana wanaojitolea (volunteers) katika
shughuli za sanaa (Arts).
Nikiwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe,
mwananchi wa Zanzibar ninayeipenda nchi yangu na pia nikiwa kama
binadamu ninayethamini utu wa kila mtu nalaani vikali na kwa nguvu zote
uovu na uhalifu huo ambao umekiuka misingi ya ubinadamu na utu.
Polisi na mamlaka nyengine za nchi zinapaswa kufanya uchunguzi wa kina
na wa haraka wa kuwajua ni nani waliohusika na tukio hili na kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria. Hili la kuchukua hatua za haraka na za
dharura na kuongeza kasi ya uchunguzi ni la muhimu sana maana sasa
matukio ya hujuma kwa kutumia tindikali (acid) yamekuwa ni jambo la
kawaida na yanaendelea kuongezeka.
Tukio hili la jana linakwenda moja kwa moja na kupiga moyo wa uchumi wa
Zanzibar kwa maana ya sekta ya utalii. Tusipochukua hatua za haraka na
za dharura na kuonekana tunajali, uchumi wa Zanzibar unaweza kuathirika
kwa kiasi kikubwa na kuyumbisha utoaji wa huduma kwa wananchi, huduma
ambazo zinategemea mapato yanayotokana na utalii.
Nilipata nafasi ya kufika haraka pale walipokuwepo waathirika wa tukio
hilo mara baada ya kupata taarifa na pia kuwasindikiza hadi Uwanja wa
Ndege wa Zanzibar nikiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii
naMichezo, viongozi wa Jumuiya ya Wawekezaji katika Sekta ya Utalii
(ZATI) na Balozi wa Heshima wa Uingereza aliyepo Zanzibar.
Nawapa pole wasichana hao wawili na nawaombea wapone kwa haraka. Fikra,
hisia na dua zetu ziko pamoja nao. Sifa ya Zanzibar kwa karne nyingi
imekuwa ni kisiwa cha amani ambacho watu wake ni wastaarabu, wakarimu na
wanaopenda wageni. Mjengeko wa jamii ya yetu ya Kizanzibari wenyewe
umetokana na mchanganyiko wa watu kutoka sehemu mbali mbali duniani
ambao walihamia Zanzibar na kupafanya ndiyo maskani yao. Kitendo kama
hichi kilichotokea jana kinakwenda kinyume na misingi ya historia yetu
hiyo.
Ni mapema kusema ni nani aliyepo nyuma ya kitendo hichi lakini jambo
moja la wazi ni kuwa yeyote anayehusika amekusudia kuiumiza Zanzibar na
Wazanzibari. Kuuhujumu utalii ni kuuhujumu uchumi wa Zanzibar na
kuyahujumu maisha ya Wazanzibari. Wakati mamlaka zinazohusika
zikiendelea na uchunguzi wa tukio hili, kuwasaka waliohusika na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, natoa wito kwa Serikali kuchukua
hatua zifuatazo:
Kuongeza doria za polisi ndani ya Mji Mkongwe ambao bado unabakia kuwa
ndiyo mji mkuu wa Zanzibar na pia kituo kikuu cha harakati zote za
kiuchumi ikiwemo biashara na utalii. Kuwepo kwa Polisi Jamii chini ya
dhana ya Ulinzi Shirikishi kusiwe ndiyo mbadala wa Jeshi la Polisi
kutekeleza wajibu wake hasa kufanya doria za kawaida.
Kuuwekea Mji Mkongwe kamera za mitaani za kufuatilia nyenendo za watu
(surveillance cameras) hasa ikizingatiwa kuwa Mji Mkongwe ndiko kwenye
harakati nyingi zinazopelekea mkusanyiko wa watu wengi wakiwemo watalii
na wageni wengine wanaotembelea Zanzibar.
Mji Mkongwe kurejeshewa huduma ya taa za njiani na za mitaa (street
lights) ili kuongeza usalama wa watu wakiwemo wageni wanaotembelea eneo
hili ambako kuna idadi kubwa ya hoteli za kitalii.
Jeshi la Polisi Zanzibar limekuwa likilalamika kwa kuwa na bajeti ndogo
isiyokidhi mahitaji ya kutekeleza wajibu wao ipasavyo ikiwa ni pamoja na
kutokuwa na usafiri wa uhakika, mafuta na vifaa vya kazi. Mamlaka
zinazohusika zinapaswa kukaa pamoja na kutatua matatizo haya.
Serikali, Jeshi la Polisi, na mamlaka nyengine zinazohusika pia
wanapaswa kuwa na vikao vya mashauriano vya mara kwa mara na Jumuiya ya
Wawekezaji katika Sekta ya Utalii (ZATI) na Jumuiya ya Watoa Huduma za
Usafirishaji na Utembezaji Watalii (ZATO) ili kushughulikia matatizo
mbali mbali yanayojitokeza hususan yale yanayohusu masuala ya usalama wa
wageni wanaotembelea Zanzibar.
Mwisho, natoa wito kwa wananchi na wakaazi wote wa Mji Mkongwe na
Zanzibar kwa ujumla kuwa makini na kufuatilia nyenendo zinazotia mashaka
au zinazoashiria mwelekeo wa kufanya vitendo vya uhalifu ndani ya Mji
wetu na ndani ya Zanzibar au hata nje ya Zanzibar na pale wanapobaini
mwelekeo kama huo kutoa taarifa haraka kwa mamlaka zinazohusika. ISMAIL
JUSSA MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI JIMBO LA MJI MKONGWE a na Jumuiya
ya Wawekezaji katika Sekta ya Utalii (ZATI) na Jumuiya ya Watoa Huduma
za Usafirishaji na Utembezaji Watalii (ZATO) ili kushughulikia matatizo
mbali mbali yanayojitokeza hususan yale yanayohusu masuala ya usalama wa
wageni wanaotembelea Zanzibar.
Mwisho, natoa wito kwa wananchi na wakaazi wote wa Mji Mkongwe na
Zanzibar kwa ujumla kuwa makini na kufuatilia nyenendo zinazotia mashaka
au zinazoashiria mwelekeo wa kufanya vitendo vya uhalifu ndani ya Mji
wetu na ndani ya Zanzibar au hata nje ya Zanzibar na pale wanapobaini
mwelekeo kama huo kutoa taarifa haraka kwa mamlaka zinazohusika.
ISMAIL JUSSA
MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI
JIMBO LA MJI MKONGWE
No comments:
Post a Comment