Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw Magesa Mulongo.
WATUHUMIWA walioingiza mabomu ya kurushwa kwa mkono yaliyotupwa Arusha Mei na Juni katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti na kwenyemkutano wa wa hadhara wa Chadema, Soweto mkoani Arusha, wamekamatwa.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema hayo jana katika mkutano wa
siku moja wa kuzungumzia fursa za uwekezaji mkoani Arusha, uliofanyika
eneo la Olasiti.
“Watuhumiwa
hawa siku si nyingi Kamanda wa Polisi wa Arusha, ataweka majina
hadharani, watu wawajue na si wageni, ila kwa sasa kinachochunguzwa ni
kutaka kufahamu waliowatuma kuingiza mabomu hayo na kwa lengo gani."
Mulongo
alisema kwa sasa Polisi iko katika hatua za mwisho za mahojiano na
watuhumiwa hao, ambapo mbali na kutaka kufahamu waliowatuma na malengo
yao, pia wanatarajia kupata taarifa za waliorusha mabomu hayo.
Malengo
mengine kwa mujibu wa Mulongo ni kuwafahamu watu wote waliopewa zabuni
ya kuingiza mabomu hayo, ili hatua za kisheria zifuate.
Mulongo
aliomba wananchi waendelee kutulia wakisubiri matokeo ya Serikali na
hata wakitajwa wahusika waiachie Polisi ifanye kazi yake. Mabomu hayo
yalirushwa Mei 5 kanisani Olasiti na Juni 15 uwanja wa Soweto, wakati wa
hitimisho la kampeni za udiwani za Chadema mkoani hapa.
Kanisani
Mlipuko huo ulitokea muda mfupi baada ya kuanza kwa ibada ya uzinduzi
wa Parokia hiyo, ambayo mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Vatican nchini na
Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu Fransisco Mantecillo Padilla.
Mbali
na Askofu Padilla, pia alikuwapo mwenyeji wake Askofu Josephat Lebulu
wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha na waumini zaidi ya 2,000.
Wakati
mgeni rasmi akitoka nje ya Kanisa akijiandaa kukata utepe kama ishara
ya uzinduzi, mtu alirusha kitu chenye ukubwa wa ngumi, kwenda eneo lenye
mkusanyiko wa watu na baada ya kutua, kulitokea kishindo na mlipuko
mkubwa uliosababisha taharuki miongoni mwa waumini na kusababisha watu
kukimbia ovyo.
Katika
tukio hilo, watu wawili walifariki dunia, akiwamo Regina Kurusei (45),
mkazi wa Olasiti aliyefariki dunia siku ya tukio wakati akipewa matibabu
katika hospitali ya Mount Meru na majeruhi mwingine James Gabriel (16)
alifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 6.
Bomu
hilo lililipuka Juni 15, katika Uwanja wa Soweto wakati wanachama na
wapenzi wa Chadema wakiwa wamekusanyika kufunga kampeni za uchaguzi
mdogo wa madiwani mkoani humo.
Mlipuaji
alilipua bomu hilo dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa,
Freeman Mbowe, kumaliza kuhutubia mkutano huo na kuhudhuriwa na mamia ya
wananchi kisha kuacha maswali mengi.
Mulongo
alitaja waliopoteza maisha kuwa ni Judith Mushi (46) ambaye alikuwa
Katibu Kata wa Chadema, Kata ya Sokoni One na mkazi wa eneo hilo
aliyemtaja kwa jina moja la Justine (16) wa Sombetini ambaye alifariki
dunia katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Siasa
Akizungumza katika mkutano huo wa kukaribisha wawekezaji jana, Mulongo
alisisitiza Serikali inahitaji siasa zenye tija na anapotokea mwanasiasa
mwenye kupinga maendeleo, atashughulikiwa.
“Kila
mwanasiasa awe wa kuchaguliwa au kuteuliwa, aliposimama kuomba nafasi
hiyo wote waliahidi maendeleo kwa wananchi, hivyo tufanye hivyo,”
alisema.
Mulongo
alisisitiza kuwa kutokana na umakini wa vyombo vya usalama, wanaomba
wawekezaji wasiwe na hofu, wajitokeze kuwekeza maeneo ya mkoani hapo,
bila hofu.
Alisema
mkoa huo unatangaza fursa za uwekezaji kwa sababu ya kuongeza kipato na
ajira kwa wakazi wa Jiji hilo pamoja na kupanua wigo wa masoko na
bidhaa zinazozalishwa hapa.
-Habari leo
-Habari leo
No comments:
Post a Comment