Thursday, February 28, 2013

Matukio ya Kisiasa

Waumini wamuaga Benedikt wa 16 Roma

Waumini kutoka Bavaria,wakishirikiana na wenzao kutoka kila pembe ya dunia wamuaga kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni
Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni, Papa Benedikt wa 16 atakaestaafu kuanzia february 28 na kujishughulisha zaidi na ibada na kutafakari,anaongoza misa yake ya mwisho katika uwanja wa Mtakatifu Petro,wakihudhuria zaidi ya waumini laki moja na nusu kutoka kila pembe ya dunia.Wakaazi wa jimbo la kusini mwa Ujerumani Bavaria anakotokea kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni wamekuja kwa wingi kumuwaga jamaa yao.
Katika misa yake hiyo ya mwisho ya hadhara kama kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,Papa Benedikt wa 16 akiwa ndani ya gari maalum la Vatikan anawaamkia umati wa waumini waliojazana katika uwanja wa Mtakatifu Petro,muda mrefu zaidi kuliko kawaida yake kabla ya kuwakaribisha kwa mazungumzo baadhi ya viongozi ikiwa ni pamoja na rais Ivan Gasparovic wa jamhuri ya Slovakia.
Miongoni mwa waumini hao kuna wale wanaotokea katika jimbo la kusini la Bavaria,wakibeba bendera za jimbo hilo na kupiga muziki wa Bavaria ambao mwenyewe Joseph Ratzinger anapenda kuusikia uklichezwa.
Tangu siku kadhaa zilizopita,umati wa waumini kutoka Ujerumani wamekuwa wakimiminika mjini Roma.Wenyewe wanasema hata akiacha wadhifa huo kesho february 28,ataendelea kuwa muhimu kwao.
Tobias Eichinger aliyekuja Roma pamoja na mchumba wake Cornelia anasema:"Tunataka kumuombea Papa mtakatifu ambae ni wa kutoka Bavaria na pia ni mwenzetu, kila la kheri .
Tobias Eichinger anasema ingekuwa vyema Joseph Ratzinger, atakapostaafu,kama kwa mfano atamtembelea kakaake Georg anaeishi katika eneo la Regensburg.Hilo litawafurahisha maelfu ya waumini wa kikatoliki na sio mie peke yangu anasema na kuungama wakati huo huo kutokana na sababu za usalama jambo hilo pengine halitowezekana.
Muhimu ni imani ya dini na sio kabila
Uwanja wa Mtakatifu Petro umejaa umati wauamini mjini Roma

Mbali na kundi hilo la wabavaria,katika uwanja wa mtakatifu Petro kuna prista wa kutoka Mexico pia anaeimba na kundi lake.Wamebeba magitaa na akordeon na watu waliowazunguka wanaitikia.Mbali kidogo kutoka mahala hapo kuna kundi la kwaya la vijana kutoka Ufaransa,bendera za Poland na Brazil zinapepeya na kila pembe yanaonekana mabango yalioandikwa kwa lugha tofauti "Ahsante Benedikt.,"
Mshika bendera wa kundi la waumini wa Bavaria Helmut Jawurek anahisi uamuzi wa Papa Benedikt wa 16 kimsingi ni sawa.Anasema ataendelea kuwa mtiifu kwa kiongozi mwengine wa kanisa katoliki ulimwenguni atakaechaguliwa na makadinali mwezi ujao wa March.Anasema tunanukuu"Kanisa katoliki ni kanisa la dunia na uraia si muhimu,la muhimu zaidi ni imani."
Mwandishi:Riegert Bernd/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charles

No comments: