Sababu za Vijana Kujingiza katika Tabia za Hatari na Namna ya Kuwasaidia
Katika makala hii tunashirikisha namna ya kuwasaidia vijana ili
waweze kuvuka vikwazo vinavyoweza kuwafanya wasifikie malengo
waliojiwekea maishani mwao. Tunatambua kwamba, yapo mambo mengi
yanayoweza kuwachelewesha au kuwakwaza vijana kutofikia malengo yao ya
maisha. Baadhi yake ni kama:
Dawa za kulevya
Ulevi
VVU/Ukimwi
Mimba kabla ya wakati, n.k.
Katika makala hii, tunaelezea sababu chache zinazopelekea vijana
(wasichana) kupata mimba kabla ya wakati. Pia tunapendekeza namna ya
kuweza kuwasaidia ili wasijikute katika mtego huu na pia waweze kufikia
malengo yao katika maisha yao. Ingawa sababu hizi zinawalenga wasichana
moja kwa moja, hata hivyo zinaweza kutumika kwa wavulana pia, kwa vile
wavulana wanajiingiza katika mambo haya kirahisi kuliko wasichana.
Bi. Tricia M. Davis amefanya utafiti kati ya wasichana wapatao 500 wenye
umri wa miaka chini ya 19, waliowahi kupata mimba zaidi ya mara moja.
Katika utafiti wake anaeleza sababu saba zilizojitokeza na kuchangia
katika hawa kupata mimba zaidi ya mara moja. Katika makala yake, “An
Examination of Repeat Pregnancies Using Problem Behaviour Theory”,
iliyochapishwa katika Jarida la Journal of Youth Studies (Vol. 5,no.3,
2002, pp.337-351), anafafanua kwa kina juu ya tatizo hili. Hivyo
tunaamini kuwa baada ya kupitia maelezo haya, kama walezi wa vijana
tutakuwa na upana wa mawazo na kuwawezesha vijana namna ya kupanga
malengo mazuri katika maisha yao na jinsi watakavyoweza kuyafikia
malengo hayo.
1. Kutokuwa na Malengo ya Maisha
Sababu ya kwanza, kati ya saba zilizoorodheshwa ni kutokuwa na malengo
maalum katika maisha. Vijana wenye malengo endelevu katika maisha huwa
wanachelewesha tendo la ndoa na hivyo kutopata mimba kabla ya wakati.
Kijana anapokuwa amejiwekea malengo makubwa katika maisha yake, hakika
atakuwa makini zaidi na daima atajiepusha na tabia zinazoweza kumpelekea
kutofikia malengo yake. Kwa mfano, ikiwa kijana fulani aliye katika
kidato cha kwanza (Form I) na ana lengo la kuwa rubani wa ndege au
kiongozi mashuhuri katika nchi au mtu yeyote maarufu, ni wazi
atajishugulisha zaidi na mambo ya masomo. Hali hii haina maana kwamba
hatajihusisha na starehe zinazoambatana na ujana! La hasha. Ila hata
kama anakwenda disko basi atatambua lengo lake na atajua dosari
inayoweza kumpata endapo atajilegeza na kufuata vishawishi vya ndani ya
disko. Kwake atatambua kirahisi kuwa akifanya ngono anaweza kupata mimba
na hivyo kushindwa kufikia malengo yake. Msichana mwenye lengo kuu kama
hili ni tofauti na yule asiyekuwa na malengo. Msichana asiyejua la
kufanya baada ya kumalizia shule ya msingi ni rahisi kwake kujiingiza
katika tabia za hatari. Hali halisi ya vijana wengi wa Afrika Mashariki
ni kuwa hawana uhakika na maisha baada ya shule ya msingi. Kwa hiyo,
sisi ambao tunahusika na malezi ya vijana tutambue kwamba njia rahisi ya
kuwawezesha vijana kutokupata mimba, wala kujiingiza katika tabia za
hatari, haitoshi kuwaambia “muwe wazuri”, bali kuhakikisha kuwa wanaweka
malengo makuu katika maisha yao.
2. Kutojithamini ya Kutosha
Hii ni hali ya kijana kujiona hafai kwa chochote katika familia
anamotoka au katika jamii ya watu inayomzunguka. Hisia hii inampelekea
kujichukia na kupata msukumo wa kutaka kutafuta thamani ya nafsi yake
kirahisi. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kujaribu mambo ya mapenzi.
Kwa msichana wa hali hii ni rahisi kufikiri thamani yake inatokana na
tendo hili la ngono kwani linaambatana na lugha nzuri wanazotumia
wavulana na ahadi au zawadi anazoweza kupewa. Wasichana wanaotoka katika
familia zisizo na upendo wa kweli kati ya wazazi (baba na mama) ni
rahisi kudanganyika na kutafuta thamani zao nje ya familia. Au mzazi
hasa baba, anayetumia lugha ya ukali daima au lugha ya mfumo dume
humfanya binti kutojisikia wa thamani. Na hali ile ya kupendwa
inapokosekana nyumbani, basi ni wazi msichana huyu anapokutana na
mvulana mwenye maneno matamu anaweza kudanganyika kirahisi. Pia
misamiati kama, “kulizaliwa kwa bahati mbaya” na nyingineyo inaweza
kupelekea kwa binti kutojipenda. Ikumbukwe kwamba nyumbani ni shule ya
kwanza ambapo kila mmoja wetu anajifunza maana ya utu na namna ya
kupenda na kupendwa na wengine. Kwa upande wa msichana, baba ndiye
mwanamume wa kwanza anayetokea kuhusiana naye, hivyo ana jukumu la
kujenga thamani ya huyu binti anayekua. Hivyo ni dhahiri kwamba kama
tunapenda kuwasaidia vijana kutokupata mimba kabla ya wakati, ni bora
kuhakikisha kama kijana fulani anathamini utu wake. Tunaweza kuwasaidia
vijana kwa kuandaa semina zinazohusu kujitambua na kuwasaidia kuanza
safari ya kutafakari, “Mimi ni nani?,” na “Thamani yangu inatokana na
nini?” Hii itawasaidia kutambua kwamba thamani ya mtu haitegemei watu
wengine wala wanavyosema, hata si umbo alilo nalo, bali ni hali ya
ndani. Thamani ya mtu ipo ndani ya utu wake, yaani nafsini mwa mtu
mwenyewe.
3. Kutowajibika
Sababu nyingine inayoweza kumpelekea kijana kupata mimba kirahisi ni
kutokuwa na tabia za kuwajibika (External locus of control).
Kutowajibika kuna maana ya mtu anavyoeleza matukio mbalimbali ya maisha
yake na jinsi gani anavyojiepusha na tukio lile. Tabia hizi zaweza
kuonekana hata katika mambo madogo madogo. Kwa mfano, kijana akidondosha
kitu fulani na kusema, “Kitu hiki kimedondoka”, yeye anajaribu
kutafsiri tukio lile kuwa hakuhusika nalo kabisa. Au mwingine
anapovunja glasi na kusema, “Glasi imevunjika” anajaribu kutowajibika na
tukio hilo. Sote tunatambua jinsi Adamu alivyotaka kujiepusha na
kutokuwajibika kwa kosa alilofanya katika bustani ya Edeni. Mungu
alipomuuliza, “Umefanya nini?” Adamu alimjibu Mungu, “Mwanamke uliyenipa
ndiye alinidanganya nami nikala…” Adamu hakutaka kuwajibika na tendo
lake. Hali kadhalika kijana mwenye mazoea ya kutowajibika katika mambo
madogo madogo, ni rahisi kwake kujiingiza katika ngono na hatimaye
kupata mimba bila kujali au kuwajibika. Wasichana wenye tabia ya kusema,
“Shetani alinidanganya” au “Tulikuwa tunajaribu,” wanaonyesha dalili za
kutowajibika na tendo walilofanya. Ni dhahiri kwamba msichana wa namna
hii hajajifunza kutokana na kosa la mwanzo, hivyo ni rahisi kwake
kurudia kitendo hicho hicho. Sisi kama walezi wa vijana tunahitaji
kuanza kuwazoesha vijana tulio nao kuwajibika katika mambo madogo
madogo. Kupendekeza kwa wazazi, walezi, na vijana wenyewe kwa kuwapa
nafasi za kujaribu shughuli zinazoendana na umri wao, na hasa katika
kumiliki vitu vyenye thamani ndogo. Hii itawafanya kujisikia kuwa wenye
kuchukua hatamu ya maisha yao.
4. Ukosefu wa Uchaji
Ukosefu wa uchaji ni ile hali ya kijana kutojali mambo ya kiimani.
Vijana wanaokuwa na hali hii ya kutojali mambo ya kidini na imani kwa
ujumla wanajiweka katika mazingira rahisi zaidi ya kujiingiza katika
tabia za hatari. Hii ni kwa sababu wanakuwa wamezamisha dhamiri zao
zisiwasumbue wanapokuwa wamekosea. Kwa upande mwingine, vijana
wanaojihusisha na vikundi mbalimbali vya kukuza imani, wanapata malezi
mazuri juu ya dhamiri zao na hivyo hata kama wakikosa ni rahisi kwao
kurudi katika msingi mzuri wa maadili. Vikundi hivi ni kama vile vya
kutafakari Neno la Mungu, fokolare, vikundi vya kiutume na vinginevyo.
Uchaji hapa si kuja kanisani Jumapili kama sheria fulani, bali ni ile
hali ya kuguswa na Mungu; kuwa na mang’amuzi binafsi ya upendo wa Mungu.
Uchaji hapa si tendo la kurudia rudia sala fulani, bali ni hali ya
kutafakari na kujiweka katika hali ya kuunganika na Mungu. Vijana wenye
mazoea haya wanajenga polepole ndani yao uwezo wa kuchunguza dhamiri na
kutathmini siku ilivyokuwa kabla ya kulala (Examination of coscience).
Hata katika sala binafsi wanaweza kugundua kosa dogo walilolifanya
katikati ya siku bila wao kujua kwa sababu ya mahangaiko ya maisha. Hali
ya namna hii inaweza kutumika kama kinga kwa makosa makubwa kama tabia
za hatari tunazozizungumzia katika makala hii.
Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kupendekeza mpango fulani utakaohakikisha
vijana wanapata fursa ya kujituliza na kutafakari maisha yao ya kiroho.
Katika matoleo ya Mlezi yaliyopita, tumewahi kuzungumzia juu ya maisha
ya kiroho kwa vijana. Tunaweza kurejea na kuona namna gani tunaweza kuwa
na mpango utakaowasaidia kuanza safari hii ya kuwa na uchaji.
5. Mazingira Duni ya Nyumbani
Hii ni sababu nyingine inayoweza kuwapelekea vijana kujiingiza katika
tabia za hatari. Kama msichana anaishi na mzazi mmoja, kuna uwezekano wa
binti kupata mimba mapema kutokana na kuathiriwa na mfano wa muundo wa
familia anayoishi. Pia kwa wale wanaotoka katika familia ambazo mume na
mke si waaminifu, kuna uwezekano mkubwa wa kijana kushawishika na kuanza
mambo ya mapenzi mapema. Hata hivyo, vijana wanahitaji kusaidiwa
namna ya kuzipokea familia zao, na kuamini kuwa si lazima waige mfano
potovu wa wazazi wao. Zaidi ya hayo, ni kutambua kwamba kuna mambo
wanayoweza kuyabadili na mengine wanahitaji kukubali nayo. Ni lazima
vijana wajue hawawezi kutawala tabia za wazazi wao ila wanaweza kukabili
tabia zao wenyewe. Kwa kufanya hivyo wanakuwa mashujaa wa mazingira
magumu waliyojikuta nayo.
6. Mshinikizo wa Rika
Mshinikizo wa rika unaweza kuwalazimisha vijana lakini si kwa sehemu
kubwa! Vijana wanaweza kushawishika kufanya ngono au kujiingiza katika
tabia za hatari kutokana na hadithi zinazosimuliwa na wenzao. Kila mmoja
hujidai kuwa alijaribu mambo haya na kuelezea jinsi alivyojisikia. Hali
hii inaweza kuchochea hamu ya kutaka kujaribu mambo yale ya hatari.
Kama kijana tayari ana malengo na anajithamini si rahisi sana
kupeperushwa na upepo huu wa masimulizi haya. Lakini kama kijana hana
malengo maalum katika maisha na hajui thamani yake, basi ni wazi
mshinikizo wa rika una nafasi kubwa ya kumpotosha.
7. Tabia ya Kupenda kujaribu mambo mapya
Vijana wenye tabia ya kupenda kujaribujaribu ili kujua ladha yake hata
bila kujali madhara yake wanaweza kuingia katika mtego kirahisi. Kwa
kufikiri kuwa wanaweza kujaribu tendo lolote la hatari mara moja tu na
kuacha, kumbe kunaweza kuwa mtego wa kudumu. Hata mara moja inaweza
kuwa mara nyingi. Kuna methali ya Kiswahili inayosema, ‘Mwonja asali
haachi kuchonga mzinga.’ Vijana wanatakiwa kueleweshwa kuwa kila tabia
inaanza kwa tendo moja la awali.
Hitimisho
Sababu zilizotolewa hapa juu zinaweza kutumika kama kinga ya kuwasaidia
vijana kutojiingiza katika tabia za hatari – kama vile utumiaji wa
madawa ya kulevya, ulevi, na kupata mimba kabla ya wakati. Basi, vijana
wasaidiwe kuwa na…
Malengo ya maisha
Hali ya kujithamini
Tabia ya kuwajibika
Uchaji
Uwezo wa kutokuzamisha na mazingira duni ya nyumbani
Msimamo wa kutofuata mkumbo, na
Uvumilvu wa kutoanza tendo lisiloendana na hali ya maisha.
No comments:
Post a Comment