LICHA ya serikali kuyapiga marufuku maandamano yaliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuishinikiza kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake wajiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne 2012, chama hicho kimesema yapo pale pale.
Chama hicho kimewaomba wananchi wote waliochoshwa na
kufelishwa kwa watoto wao, kunyimwa elimu bora wajitokeze kuandamana kwa
nguvu zote, na wanafunzi wote waliofeli pia wajitokeze kudai elimu bora
kwani ni haki yao.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana na
kutoa msimamo huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema
“wananchi wajitokeze kwa wingi ili kilio chao kisikike duniani kote.”
Alisisitiza
kuwa maandamano hayo yatafanyika mbele ya ugeni wa Rais wa China, Xi
Jinping ili kufikisha kilio hicho na kamwe haikubaliani na sababu ya
serikali kuyazuia kwa sababu ya ugeni huo.
Alisema maandamano
hayo yatasaidia kupuuza kunakofanywa na Serikali ya CCM kuonwe na dunia
nzima maana vyombo vyote vya habari vitafuatilia tukio hilo.
Mbowe
aliongeza kuwa, “Watanzania waliochoshwa na ubabaishaji katika elimu
wajitokeze, kulaani kitendo cha Waziri Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu
wake, Philipo Mulugo kulindwa na serikali, badala ya kuwajibishwa kwa
matokeo mabaya ya watoto wa Kitanzania.”
Alipoulizwa itakuwaje
maana kutakuwa na ugeni wa Rais wa China nchini, sababu ambayo hata
serikali imeitumia ili kuyazuia maandamano hayo, Mbowe alijibu: “Kilio
chetu hakikuja na Rais wa China, kama Serikali ya CCM wanaona aibu
kumwajibisha waziri mmoja na naibu wake, basi wasubiri aibu ya dunia
kuona jinsi Tanzania inavyoendeshwa kibabe, ikiwa haina elimu bora.
“Tumetangaza
maandamano wiki tatu zilizopita, hatukuwa na taarifa na ujio wa Rais wa
China, lakini jinsi Mungu alivyo upande wetu amemleta Rais wa China,
kweli Mungu ni mwema, hakuna tena nafasi ya kusubiri kuficha ubovu
katika sekta ya elimu nchini, ndani ya siku ambayo CHADEMA waliandaa
maandamano ili dunia nzima isikie kilio cha Watanzania kuhusu elimu.
“Sababu
kuwa CCM nao wameandaa maandamano kupinga maandamano ya CHADEMA hazina
msingi ni kutowajibika kwa Jeshi la Polisi. Hatukatazi maandamano,
polisi wapange ratiba siku tofauti, sisi tutaandamana kumpinga waziri
ili kama CCM wataandamana kumpongeza waziri wao wapangiwe siku yao, ila
sisi tulitangaza mapema na barua tulipeleka kwa mujibu wa sheria za nchi
yetu.”
Alipoulizwa kwanini asisubiri Tume ya Waziri Mkuu itoe
majibu, Mbowe alisema: “Hatuna shida na Tume ya Waziri Mkuu, matatizo ya
elimu katika nchi yetu yapo wazi, tukizungumza bungeni wanatuchakachua,
na sasa huku nje wanatukejeli, tunataka ifike mahali wajue kuwa nchi
hii ni yetu sote, na Watanzania wanapaswa kusikilizwa kilio chao.”
Kwa
mujibu wa Mbowe, maandalizi ya maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika
katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, yamekamilika.
Jana,
Idara ya Habari (Maelezo) ilitoa barua iliyosainiwa na mkurugenzi wake,
Assah Mwambene kuzuia maandamano yaliyokuwa yafanyike Jumatatu ijayo
katika mikoa ya Mbeya na Arusha tu.
Taarifa hiyo haikuzungumzia maandamano yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam wala Mwanza.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, serikali ilisema kuwa maandamano ya
CHADEMA yalipangwa kuhusisha wananchama kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa,
Njombe na Ruvuma, na kuongeza kuwa CCM ilipanga kufanya maandamanno yake
mkoani Arusha kupinga kusudio la CHADEMA kuandamana, wakieleza kwamba
wana imani na tume maalumu ya Waziri Mkuu inayochunguza tatizo la
kufanya vibaya wanafunzi wa kidato cha nne.
Awali CHADEMA
walitangaza maandamano yatakayofanyika katika kanda nne. Kanda ya Kusini
yatafanyika Mbeya; Kanda ya Ziwa yatafanyika Mwanza; Kanda ya Kaskazini
yatafanyika Arusha, na Kanda ya Mashariki yatafanyika Dar es Salaam.
Tanzania
Daima ilipomuuliza Mkurugenzi wa Maelezo imekuwaje yeye akawa msemaji
wa jambo hili, alijibu: “Mimi ni msemaji wa serikali, hata Ikulu
naisemea, hivyo usiulize kwanini naisemea polisi.”
Sababu
nyingine iliyotolewa na serikali kupitia Maelezo ilisema ni kwa sababu
siku hiyo ni muhimu kwa Watanzania kumpokea Rais mpya wa China ambaye
atakuwa na ziara ya siku mbili nchini.
Februari 19 mwaka huu
akiwa jijini Mwanza, Mbowe alitoa siku 14 kwa Waziri Kawambwa kujiuzulu
kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne.
Kauli
hiyo ilitolewa siku moja baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA)
kutangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 ambapo asilimia sitini ya
wanafunzi wote waliofanya mtihani wamefeli.
Gazeti la- Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment