Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji na Uwekezaji DKT. Mary Nagu
(katikati) akifurahia jambo na viongozi wa makampuni ya china (kushoto)
ni Mkuu wa chama cha ushirikiano cha China Bw. Charles Li wakiwa
wanaonyesha bango lenye maandishi ya lugha ya China kuonyesha
ushirikiano kati ya China na Tanzania (kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi wa
WCUGA International Group Bw. Tiger Liang.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) Bw. Raymond
Mbilinyi (kushoto) akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Uwekezaji na Uwezeshaji, DKT. Mary Nagu wakielekea katika ukumbi wa
kivukoni katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam juzi jioni kuonana
na ujumbe wa wawekezaji wa china kwa ajili ya kujadili namna ya
kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji hapa nchini. Ujumbe huo wa
makampuni kumi na tano toka nchini China uliongozwa na Mkuu wa chama cha
ushirikiano cha China Bw. Charles Li.
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Serikali
Imesema itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wawekezaji
wa ndani na nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kutanua wigo wa huduma za
jamii na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji ,
Dkt. Mary Nagu aliuambia ujumbe wa makampuni kumi na tano kutoka nchini
China, uliokuja kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji hapa nchini kuwa
serikali ina mkakati kabambe wa kuendelea kuboresha mazingira ya
uwekezaji.
“Serikali
na bajeti yake haitoshi kuwapa watanzania mahitaji yao ya ajira na
huduma za jamii, pale ambapo kuna mradi unaleta faida kwa mwekezaji
lazima tuhakikishe tunawachia wawekezaji ili fedha za bajeti ya serikali
ziende kwenye huduma nyingine za jamii kama elimu” alisema Waziri Nagu
katika chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa wawekezaji hao jijini Dar
es Salaam juzi usiku.
Alisisitiza
kuwa kama kuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya barabara na hapo
hapo kuna mwekezaji anataka kuwekeza katika sekta hiyo ni bora
wawekezaji wapewe hiyo fursa ili serikali ielekeze nguvu katika sekta
nyingine ambazo zinahitaji uwekezaji katika kusaidia wananchi.
Akizungumzia
ujumbe wa makampuni kumi na tano ya kutoka nchini china, Waziri Nagu
alisema wamepata moyo wakuja kuangalia fursa mbalimbali za kiuwekezaji
kutokana na agizo la Rais wa nchi yao Bw. Xi Jin Ping kutembelea hapa
nchini.
“Kutokana
na maagizo ya Rais wa China kwamba wamewekeza katika nchi nyingine,
sasa wakati umefika kuwekeza katika bara la Afrika hasa kwa nchi ya
Tanzania, hivyo ni fursa ya kipekee kwa watanzania kutoa ushirikiano
katika kufanya kazi na watu wa china”, alisisitiza DKT. Nagu.
Aliongeza
kuwa lililo muhimu kwa sasa ni wawekezaji kuelekezwa kwenye faida, na
ndio maana ameonana na ujumbe wa makampuni hayo na kuwaambia kuwa kuna
fursa mbalimbali hapa nchini ambazo wakiwekeza watapata faida na nchi
pia ifaidike kutokana na rasilimali zake.
“Naomba
nichukue nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji hawa kutoka china waone
fursa hizi na fursa zipo wazi, kazi ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC)
ni kuwezesha wawekezaji waweze kuwekeza na kuona Tanzania inapata
manufaa ya ajira, kodi itaongezeka na uchumi utakuwa”, aliongeza.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Raymond Mbilinyi,
alisema mara baada ya kukutana na makampuni hayo yapatayo kumi na tano,
tayari yameonyesha nia ya kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali hapa
nchini.
“Baada
ya kukutana na taasisi za serikali na zile za binafsi makampuni haya
yameonyesha nia ya dhati kuwekeza katika maeneo ya Elimu, Umeme, miundo
mbinu, kilimo na afya” alisema Mbilinyi.
Aliongeza
kuwa China ni moja ya nchi ambazo zinaongoza kwa uwekezaji hapa nchini,
ikiwa ni nchi ya nne katika kuwekeza, huku akisisitiza kuwa baada ya
muda mfupi inaweza kuwa nchi ya kwanza kutokana na juhudi kubwa
inazofanya katika eskta hiyo.
“Sisi
TIC inatupa moyo sana na hii ni kutokana na viongozi wetu wawili Rais
Jakaya Kikwete na Rais wa China Xi Ji Ping kuonyesha njia na nia ya
dhati, hivyo sekta binafsi kutoka China na Tanzania zitaweza kuwekeza
kwa kasi katika Taifa letu”, aliongeza Kaimu Mkurugenzi huyo wa (TIC).
No comments:
Post a Comment