WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaitisha kikao cha wadau
mbalimbali kutoka taasisi za dini, mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja
na vyama vya siasa ili kujadili mustakabali wa Taifa la Tanzania na
hasa suala la amani na utulivu.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Machi 20, 2013) wakati wa
mahojiano maalum na kituo cha Redio Vatican kilichopo Vatican City,
mjini Roma, Italia.
“Serikali
inatarajia kuitisha kikao cha wadau wote kutoka vyama vya siasa,
mashirika ya dini, NGOs, ili kutafakari nini kifanyike ambacho
kitasaidia kuendeleza amani na utulivu... tutaitisha kikao hiki tarehe 4
Aprili,” alisema Waziri Mkuu wakati akihojiwa na Padri Richard Mjigwa,
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Akijibu swali kuhusu kuwepo kwa vurugu
na mauaji ya viongozi wa kidini nchini Tanzania, Waziri Mkuu Pinda
alisema Serikali imechukua hatua za kisheria kwa kufanya uchunguzi wa
kina kwa kila eneo na baadhi ya wahusika kufikishwa mbele ya vyombo vya
sheria. Alisema kwamba juhudi kubwa bado zinaendelea kuwasaka wahusika
wa mauaji ya Padre Evarist Mushi aliyeuawa Visiwani Zanzibar.
Akiwa
katika studio hizo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza
Watanzania waliko ughaibuni ambao wanaisikiliza redio Vatican kwa njia
ya mtandao ama redio hatua ambayo mchakato wa uundaji katiba mpya
imekwishafikia kwa sasa.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania
na watu wenye mapenzi mema washikamane na waendelee kumwombea Papa
Francis wa Kwanza ili aweze kufanikisha kazi ambayo amepewa na Mwenyezi
Mungu aikamilishe.
“Ninamshukuru
Mungu kwa kumteua mtu anayeamini ataliongoza Kanisa Katoliki… atasaidia
kuimarisha utangamano wa dunia nzima, tuendelee kumuombea akamilisha
kazi kubwa aliyopewa na Mwenyezi Mungu,” alisema.
“Ujumbe
alioutoa kwenye misa ya jana umenigusa sana na hasa msisitizo wake wa
kutaka kila mmoja wetu aone atawasaidiaje watu maskini… watu
wanaotengwa, watu wanaonyanyaswa na watu wanaonyanyapaliwa”, aliongeza.
Waziri
Mkuu alikuja Roma, Italia kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye ibada
maalum ya kumsimika Papa Francis iliyofanyika kwenye juzi (Jumanne,
Machi 19, 2013) kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mt. Petro mjini
Vatican.
Waziri
Mkuu alisema ameguswa mno na Papa Francis wa Kwanza kwani ni kiongozi
ambaye ametoa changamoto ya kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea
maskini na wote wanaoonewa ili waweze kuondokana na baa la umaskini.
Idhaa
ya Kiswahili ya Redio Vatican iko kwenye studio ambayo ilikuwa ikitumiwa
na Baba Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili kupeleka ujumbe kwa waumini
wote ulimwenguni. Radio Vatican ambayo inaendesha idhaa za lugha
nyingine kadhaa za kimataifa, ina wafanyakazi 500 na ina programu 45
zinazoandaliwa na redio hiyo.
No comments:
Post a Comment