Uendeshaji
wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa kwa mujibu
wa Sheria ya Utumishi wa
Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007
kifungu 29 (1). Jukumu la msingi la Sekretarieti ya Ajira ni kuendesha mchakato
wa ajira katika Utumishi wa Umma. Hapa
ina maana kuwa jukumu la kuajiri,
kuthibitisha watumishi kazini pamoja na masuala ya nidhamu ya Watumishi
yanabaki kwa Watendaji Wakuu wa Wizara na Taasisi katika Utumishi wa Umma mitarafu ya Kifungu cha 6(1) (b) cha Sheria
ya Utumishi wa Umma no 8 ya mwaka 2002. Ambapo katika kuendesha mchakato huo,
Sekretarieti ya Ajira inapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu zilizopo
ili kuhakikisha Utumishi wa Umma unapata Watumishi weledi na wenye maadili
mema. Ambapo hadi sasa jumla ya waombaji 4891 tumeshaendesha mchakato wao wa
ajira na kuwapangia vituo vya kazi. Hata
hivyo, Sekretarieti ya Ajira kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma ilipeleka Mswada Bungeni unaopendekeza kukasimu madaraka ya
kuendesha mchakato wa Ajira ili baadhi ya Waajiri wakasimiwe madaraka hayo ili
kurahisisha utendaji kazi katika kushughulikia
mchakato wa ajira kwa baadhi ya kada. Huku Sekretarieti ya Ajira
ikiendelea kuhakikisha kuwa jukumu hilo linaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.
Tunapoongelea suala la ufanisi hapa Kitengo cha Udhibiti na Ubora kinasimamia
suala zima la uhakiki wa taarifa za mhusika, uhakiki wa vyeti na uadilifu wake
kwa ujumla. Ambapo hadi sasa tumeshabaini
jumla ya vyeti vya kughushi 677 ambavyo wahusika wanadai wamevipata
kutoka RITA, VETA na NECTA.
Nafasi wazi za kazi zitakazokuwa zikitangazwa na
mchakato wake kuweza kukasimiwa ni pamoja na Kada ya Wasaidizi wa ofisi,
Wahudumu wa afya, Madereva, Maafisa Watendaji wa Kata, Mtaa, Kijiji, Wapishi,
Walinzi, Madobi, Wasaidizi watunza kumbukumbu pamoja na Makatibu Muhtasi (walio
chini ya cheo cha mwandishi mwendesha ofisi)
au Kada zingine ambazo Katibu wa Sekretarieti ataona inafaa kukasimu.
1
Aidha, nitoe ushauri kwa
wanafunzi walioko shuleni na wanaotarajia kuingia vyuoni kuchukua masomo ama
kozi za fani ya Afya, Elimu, Mifugo na Kilimo maana ni maeneo ambayo bado yana
fursa nyingi za ajira Serikalini na wahitimu wake pindi wamalizapo wanapangiwa
vituo vya kazi moja kwa moja bila ya kupitia mchakato wetu wa ajira kutokana na
uhaba wa Wataalam wa fani hizo katika soko la ajira hivi sasa.
Sekretarieti ya Ajira
katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa
kwa haraka zaidi zinazohusu
mchakato wa ajira katika Utumishi
wa Umma, pamoja na kuboresha mawasiliano kati ya Ofisi yetu na wadau ili
kuweza kuendana na mabadiliko ya sayansi na
teknolojia ya habari na mawasiliano nchini na duniani kwa ujumla,
iliamua kuanzisha tovuti yake (www.ajira.go.tz) ambayo imerahisisha kwa kiasi kikubwa utoaji na upokeaji wa
taarifa mbalimbali hususani za matangazo ya fursa za ajira taarifa
nyingine zinazohusu masuala ya ajira Serikalini na matangazo mengine yanayohusu
shughuli za Sekretarieti ya Ajira. Tangu kuzinduliwa mwezi Aprili, 2012 imeweza
kutembelewa na wadau wapatao 3,017,410
Pamoja na tovuti
Sekretarieti ya Ajira imeanzisha KANZIDATA (DATABASE) za aina tatu (3) ambazo ni Kanzidata ya
Wahitimu wa Vyuo na Watalaam weledi, Kanzidata ya waliofaulu usaili na
Kanzidata ya waliopangiwa vituo vya kazi.
Jambo lingine ambalo
ningependa mkalifahamu ni kuwa, Sekretarieti ya Ajira iko katika hatua za awali
za mchakato wa kuwawezesha waombaji wa fursa za ajira kuwasilisha maombi ya
kazi kwa mfumo wa kielektroniki (e-application) kwa nafasi wazi zitakazokuwa
zikitangazwa katika Utumishi wa Umma ili kurahisisha kupunguza mlolongo wa
uendeshaji mchakato wa ajira ulivyo hivi sasa.
Mwisho nimalizie kwa
kuwataka waombaji wa fursa za ajira kutokuchagua maeneo ya kufanyia kazi,
hususani wale wanaopangiwa vituo vya kazi na Sekretarieti ya ajira na hawaendi
kuripoti bila ya kutoa sababu za msingi maana Sekretarieti ya Ajira inaona hili
ni kosa na inaandaa utaratibu wa kutowaruhusu kufanya usaili mwingine waombaji
kama hao.
Imetolewa tarehe 12 Julai,
2013 na Riziki V. Abraham, Msemaji na
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
+255-687624975
2
No comments:
Post a Comment