Deodatus Balile.
Kuuawa kwa mpigapicha wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, kutekwa kwa Mhariri wa New Habari, Absalom Kibanda na kufungiwa kwa muda usiojulikana kwa gazeti la Mwanahalisi, kumechafua taswira ya Tanzania kimataifa, ripoti imeeleza.
Ripoti inayoitwa "Shida Isiyoonekana ya Vyombo vya Habari vya Tanzania," iliyotolewa na shirika lisilo la Kiserikali la kutetea Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (CPJ), imeitaka Tanzania kufanya uchunguzi dhidi ya mashambulizi ya Kibanda na kuwabaini waliohusika ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, ripoti hiyo imeeleza kwamba tangu kuuawa kwa Mwangosi mwaka jana, hakuna ofisa yeyote aliyewajibishwa kwa mauaji hayo.
Ripoti pia inahoji taswira ya kimataifa ya Serikali ya Tanzania ambayo inajitangaza kwa uwazi na demokrasia. Ripoti hiyo inaeleza kuwa tasnia ya habari nchini inakandamizwa na sheria 17 zinazohusu ukandamizaji wa vyombo vya habari.
CPJ katika ripoti yake, shirika hilo limependekeza wale wote waliohusika na mpango wa siri wa kumteka Kibanda na kumtesa wasakwe ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Kadhalika, Shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Marekani, limesema ufanyike uchunguzi huru dhidi ya mauaji ya Mwangosi aliyepigwa bomu mwaka 2012 eneo la Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Ripoti ya CPJ ilisema lazima uchunguzi ufanyike ili kuwabaini waliohusika na kifo cha mwandishi huyo ambao walionekana kwenye picha katika tukio hilo.
Katika taarifa yake, CPJ imeitaka Serikali ya Tanzania kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza katika sheria zake.
Ripoti hiyo ya CPJ imetolewa na imehusu mauaji na matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo waandishi wa habari wanapokuwa kazini.
Mshauri na mwandishi wa ripoti wa CPJ, Afrika Mashariki, Tawi la Nairobi nchini Kenya, Tom Rhodes, alisema katika ripoti yake kuwa Kibanda, alifanyiwa ukatili kwa kukatwa kidole, kung'olewa jicho pamoja na meno.
Ripori hiyo inasema simu ya Kibanda na kitambulisho chake cha uraia vilichukuliwa, lakini pochi yake iliyokuwa na fedha na simu aina ya iPad, viliachwa pembeni mwake baada ya kumuumiza na kumuacha hapo na kwamba tukio hilo linaonyesha kuwa kulikuwa na dhamira nyingine zaidi ya ujambazi.
“Nawezaje kurudi tena eneo ambalo hakuna uchunguzi uliofanyika, anasema Kibanda, “Bado sijajua kama walitaka kuniua ama kunitesa.”
Wakati Polisi wakisema uchunguzi wa tukio Kibanda bado unaendelea, Mwandishi Deodatus Balile, aliyeongoza uchunguzi huru kwa niaba ya Vyama vya Waandishi wa habari, amesema polisi wamesema hakuna namna ya kuwatia hatiani watuhumiwa.
Shirika hilo limetoa mtiririko wa matukio 10 dhidi ya mashambulizi kwa vyombo vya habari tangu Septemba 2012, hadi sasa likiwamo hilo la Kibanda, Mwangosi na kufungiwa kwa Mwanahalisi.
No comments:
Post a Comment