Thursday, August 8, 2013

.. SERIKALI YAVUNA AIBU KWA DK ULIMBOKA

Dk. Steven Ulimbo,  Aliyeshtakiwa juu yake hahusiki kabisaMahakama ya Kisutu yamfutia mashtaka
 , Polisi wamng'ang'ania kwa kuwadanganya.Ni kama Serikali imevuliwa nguo baada ya Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu kumwachia huru raia wa Kenya, Joshua Gitu Mhindi  (32), aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutaka  kumsababishia kifo, Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven  Ulimboka.

Hata hivyo, baada ya kuachiwa huru, alikamatwa tena na kusomewa shtaka  jipya la kutoa taarifa za uongo katika kituo cha Polisi Oysterbay,  kwamba alimteka nyara Dk. Ulimboka.

Mshtakiwa huyo alidaiwa kufanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 122, cha kanuni ya adhabu.

Raia huyo wa Kenya, aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumteka na  kujaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka, aliachiwa huru mbele ya Hakimu  Warialwande Lema na kufunguliwa shauri jipya mbele ya Hakimu Aloyce  Katemana.

Mshtakiwa huyo alisomewa shtaka hilo jipya na Wakili wa Serikali  Mwandamizi, Tumaini Kweka, ambaye alidai Julai 3, mwaka jana katika  kituo cha Polisi Oysterbay, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam,  Mulundi alitoa maelezo ya uongo kwa maofisa wa polisi, kwamba yeye  pamoja na wenzake ambao hawapo mahakamani, walimtesa na kumteka nyara  Dk. Ulimboka, taarifa ambazo siyo za kweli.

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka, na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi  wa shauri hilo umekamilika, na kuomba tarehe ya kutajwa pamoja na  kusikiliza maelezo ya awali.

Wakili Kweka aliiambia Mahakama kuwa pamoja na kwamba dhamana kwa  mshtakiwa iko wazi, Jamhuri inaomba Mahakama izuie dhamana kwa mshtakiwa  huyo kwa sababu hana makazi maalum Tanzania na sababu za kiusalama  kutokana na mazingira ya shauri hilo.

Alidai kwamba Mahakama ikimpa dhamana, itakuwa vigumu kwa mshtakiwa kujua tarehe ya kesi kwa sababu makazi yake hayajulikani.

Baada ya ombi hilo, mshtakiwa huyo alidai mahakamani hapo kuwa amekaa  gerezani tangu mwaka jana; alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili na  sasa amesomewa shtaka lingine.

“Sasa hivi wanasema nimetoa maelezo ya uongo, mheshimiwa wanataka  kunipoteza nikiwa bado ni kijana mdogo, wanataka ku-silence  (kunyamazisha), Bunge pamoja na wananchi,” alidai na kuongeza:

“Naumia kwa sababu nashtakiwa kwa kitu ambacho sikifahamu, mheshimiwa  naenda kufanya demonstration (maandamano) na mgomo gerezani, nitachukua  uamuzi ambao wewe mwenyewe utasikia.”

Hata hivyo, Mahakama ilisikiliza ombi la upande wa Jamhuri la kumnyima  dhamana mshtakiwa na kurudishwa rumande hadi Agosti 20, mwaka huu.

Julai 13, mwaka jana Mhindi alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya  kwanza akiwa anakabiliwa na mashtaka mawili. Katika shitaka la kwanza,  ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo Juni 26, mwaka jana, katika eneo la Leaders  Club, alimteka Dk. Ulimboka.

Shitaka la pili, anadaiwa Juni 26 mwaka jana, akiwa katika eneo la Msitu  wa Mabwepande Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria alijaribu  kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.

MBWEMBWE ZA POLISI BAADA YA KUMKAMATA
Julai 13, mwaka jana, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,  lilimkamata Mhindi na kumfikisha Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashtaka  ya utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili kiongozi wa Jumuiya ya  Madaktari, Dk. Ulimboka.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleman Kova, alisema  mtuhumiwa alikutwa na kitambulisho cha taifa la Kenya namba 29166938  kinachoonyesha kimetolewa Oktoba, 2010 Wilaya ya Nyeri.

Pia alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na hati ya kusafiria ya dharura  namba 0123431 inayoonyesha imetolewa Juni 14, mwaka jana Namanga Arusha.

Alifafanua kuwa mtu huyo alifika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima  lililopo Kawe, jijini Dar es Salaam ambalo kiongozi wake ni Mchungaji  Joseph Gwajima na kutaka kuonana naye bila mafanikio.

Alisema mtuhumiwa huyo alifanikiwa kuonana na Mchungaji Msaidizi wa  kanisa hilo, Joseph Kiriba na kumweleza kuwa yeye ni mwanachama wa  kikundi cha Mafia ambacho hukodiwa kufanya matukio ya kihalifu nchini  Kenya na nje ya mipaka.

Kamanda Kova alisema mtuhumiwa huyo alijieleza alikuja Tanzania na  wenzake 12, kwa lengo la kumdhuru Dk. Ulimboka, baada ya kukodiwa na mtu  ambaye hakumtaja jina, lakini anaaminiwa ni mtumishi wa serikali.

Baada ya utekelezaji wa tukio hilo, wenzake waliondoka Dar es Salaam na yeye kwenda kanisani hapo kufanya toba.

Aliongeza kuwa kufuatia tukio hilo, raia wema walitoa taarifa polisi na kufanikisha kukamatwa kwa mshtakiwa huyo.

Kamanda Kova alisema katika mahojiano ya awali mtuhumiwa huyo alidai ni  mwanachama wa kikundi cha kihalifu kinachojulikana kama Gun Star,  kilichopo eneo la Ruiru Wilaya ya Thika nchini Kenya.

Alisema mtuhumiwa huyo alimtaja mmiliki wa kikundi hicho anayejulikana  kwa jina la utani kama Silencer akisaidiana na Past, ambao wamemfundisha  matumizi ya silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya  kihalifu nchini humo.

Alisema mtuhumiwa huyo alidai kuwa kati ya watuhumiwa wenzake 12,  aliwafahamu wawili tu ambao alisafiri nao kutoka mjini Moshi kuja Dar es  Salaam kwa ajili kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka ili ataje wanaomtuma  kushawishi mgomo wa madaktari nchini.

Mtuhumiwa huyo aliliambia Jeshi la Polisi kuwa waliambiwa baada ya  kukamilisha kazi waliyotumwa, wamuue Dk. Ulimboka na waliahidiwa kulipwa  fedha nyingi ambazo hakuzitaja.

Kamanda Kova alisema katika mahojiano zaidi na mtuhumiwa huyo,  alibainisha kuwa, Juni 26, mwaka huu walisafiri kuja Dar es Salaam kwa  basi asilolikumbuka na kukutana na mwenyeji ambaye alimpeleka hoteli  moja iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Ilidaiwa siku hiyo baada ya kufika walipanga namna ya kutekeleza kazi  waliyotumwa kuifanya usiku huo, na kwamba alishindwa kuondoka baada ya  tukio kutokana na kuona kuwa kitendo alichokifanya ni cha kinyama na  kuamua kukimbilia kanisani kwa toba.

Siku chache baada ya Kova kutoa taarifa hiyo, Mchungaji Kiongozi wa  kanisa hilo, Josephat Gwajima, alikana kuwa mtu huyo alikwenda kutubu  kanisani hapo.

Mchungaji Gwajima alisema makanisa yote ya watu waliookoka hayana utaratibu wa waumini kutubu kwa wachungaji.

Pia alisema mtu huyo baada ya kukamatwa, walinzi wa kanisa hilo  walikubaliana na polisi wamwachie hasa baada ya yeye mwenyewe kueleza  kuwa ana matatizo ya akili na hivyo amekuwa na tabia ya kuropoka ropoka  hata katika mambo ambayo siyo ya kweli.

MAKINDA AZUIA MJADALA

Mwaka jana katika vikao vya Bunge, Spika Anne Makinda, alizuia mijadala  ya baadhi ya wabunge waliotaka kuihoji serikali kuhusu kutekwa kwa Dk.  Ulimboka kwa madai kuwa kulikuwa na kesi mahakamani.

Aidh, hatua hiyo ya kuachiwa mtuhumiwa huyo, inakuja wakati matukio ya  kuteswa kwa Mhariri wa New Habari, Absalom Kibanda na mauaji ya Padre  Evaristus Mushi, wa Kanisa Katoliki hajayapatiwa majibu yoyote mpaka  sasa.

Aidha, uchunguzi wa matukio mawili ya milipuko ya mabomu mkoani Arusha  nao haujapatiwa majibu licha ya Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi.

Tukio la kutekwa na kupigwa. Dk. Ulimboka, lilisababisha serikali  kulifungia gazeti la Mwanahalisi kwa madai kuwa lilikuwa limeandika  habari za uchochezi dhidi ya serikali, baada ya kutaja majina ya maofisa  wa Usalama wa Taifa waliohusika na tukio hilo.
Source:Gumzo la jiji

No comments: