Thursday, August 8, 2013

WAZAZI WAKATAZA WALIMU WASIWAFUNDISHE WATOTO WAO JINSI YA KUTUMIA CONDOM..


Imeelezwa  kuwa Baadhi ya wazazi na walezi wilayani Kahama mkoani Shinyanga  wamekuwa wakiwazuia walimu kutoa elimu ya njia ya kujikinga na ukimwi  kwa watoto wao wa sule za msingi ikiwemo matumizi sahihi ya condom.

Hayo  yamebainika leo katika semina iliyoandaliwa na shirika la UNESCO  iliyojumisha wakuu wa shule za msingi na sekondari pamoja na mashirika  yasiyo ya kiserikali iliyofanyika katika ukumbi wa Golden Valley Mjini  Kahama.

Akichangia hoja katika semina hiyo Mwalimu mkuu wa shule  ya Msingi Korogwe Bi Ashura Rugakingira amesema kuwa wamekutana na  tatizo hilo toka kwa baadhi wazazi hao licha ya kuwa somo hilo lipo  katika mtaala wa Serikali.

Rugakingira amesema kuwa changamoto  hiyo inawafanya walimu wengi kukata tamaa ya kutoa elimu hiyo ya  kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa wanafunzi hao.

Awali  akifungua semina hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Bi Isabela  Chilumba amewataka walimu hao kuvunja ukimya na kuwa wawazi kuzungumza  na wanafunzi wao kuhusu Maambukizi ya virusi vya ukimwi na UKIMWI.

Sambamba  na hayo Chilumba ametoa angalizo kwa wananchi kutodanganyika na takwimu  za maandishi zinazotolewa na kwamba kila mtu awe mstari wa mbele kupima  afya yake mwenyewe.

Naye Msimamizi wa mradi huo wa Elimu ya Afya  ya UKIMWI, uzazi na maadili kwa vijana kutoka UNESCO Mathius Herman  amesema lengo la mradi huo ni kujenga mahusiano rasmi kati ya Mashirika  yasiyo ya serikali na shule.

No comments: