&&&&&&
Inaonekana kuwa watu wengi hawajui ni kiasi gani cha kalori za
chakula tunachotakiwa kula kwa siku. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya
Kimataifa ya Taarifa ya Chakula umeonesha kuwa, nchini Marekani raia
wengi wa nchi hiyo hawafahamu vipimo vya kalori katika vyakula, ambapo
katika kundi lililochunguzwa, asilimia 12 tu ndio walifahamu kiwango cha
kalori wanachotakiwa kula kwa siku. Asilimia 43 hawakufahamu na 35
walikosea kiwango hicho. Kuna umuhimu mkubwa kufahamu kuwa, tunatakiwa
kula kiasi cha kalori sawa na kalori zinazotumiwa na miili yetu ili
kudhibiti uzito na kujiepusha na unene. Hata hivyo kuna mambo mengi
yanayoathiri kiwango cha kalori kinachotakiwa kuliwa kwa siku kama vile
jinsia, umri, uzito, urefu na aina ya kazi na shughuli za mwili. Lakini
kabla sijaendelea mbele pengine ningechukua fursa hii kuwafahamisha
wasikilizaji wetu maana ya neno kalori. Maana ya kalori kwa mujibu wa
fizikia, ni kiasi cha nishati zinazohitajika kuongeza joto la gramu moja
ya maji kwa celcius moja. Lakini tukiitafsiri kalori kwa mujibu wa
lishe na chakula, ni kiwango cha nishati ya chakula au nguvu
inayopatikana kutokana na chakula tunachokula. Kwa msingi huo kwa mfano
tunaposema kuwa, mkate una kalori 55, tunamaanisha kwamba, kiasi cha
nguvu kinachotokana na mkate ni kalori 55. Kujua maana ya kalori na
kiasi cha kalori tunachokula hutusaidia kufahamu ni kiasi gani cha
nishati miili yetu inahitajia kwa siku kwa ajili ya mahitaji yake na
hivyo kuweza kudhibiti uzito wa miili yetu kwa kutoipatia kalori nyingi
zaidi ya mahitaji yake. Suala hilo pia mbali na kuimarisha afya zetu
vilevile huzuia unene wa kupindukia tatizo ambalo linazidi kuongezeka
kila siku duniani kote.
&&&&&
Wanasayansi wanatuambia kuwa, ratili moja ya mafuta (ambayo ni sawa
na karibu nusu kilo) ni sawa na kalori 3,500, kwa hivyo iwapo mtu
atapunguza kalori 500 kwa siku, kwa wiki anaweza kupunguza ratili moja
na hivyo kupunguza uzito. Ni vigumu kujua kiasi cha kalori kinachotakiwa
kwa siku, kwa sababu kila mtu ana sifa tofauti za kimwili na pia
kiwango cha kazi na namna anavyoushughulisha mwili wake. Wataalamu wa
masuala ya afya wanatushauri kuwa, ni bora wanawake wale kalori 1,400 na
wanaume kalori 1,800 kwa siku. Pia ni bora tusile kalori zinazopungua
1,000 kwa siku, na tuzingatie kazi tunazofanya kwa siku na jinsi
tunavyoishughulisha miili yetu. Hii inamaanisha kuwa, ikiwa mtu anafanya
kazi ya kukaa chini muda mrefu isiyo nzito na kutoushughulisha sana
mwili kama vile kazi za maofisini, ni wazi kuwa kiwango cha kalori
anachohitaji kwa siku ni kidogo. Tofauti na watu wanaofanya kazi
zinazohitaji nguvu kubwa na zilizo ngumu kama vile kilimo, ujenzi, ukuli
na kadhalila ambazo huufanya mwili utumie nishati nyingi. Hivyo watu
wenye kufanya shughuli hizo ni wazi kuwa wanahitaji kula kiasi kingi
zaidi cha kalori kwa siku. Vilevile ili kudhibiti uzito wa mwili na
kujiepusha na unene wa kupindukia mazoezi yanapaswa kuzingatiwa. Hii ni
kwa sababu wakati tunapofanya mazoezi miili yetu huchoma kalori za ziada
mwilini na hupunguza unene na kuudhibiti. Hata hivyo, hatupaswi kula
kalori chache kuliko mahitaji ya miili yetu na ni bora kutopunguza
kalori zaidi ya 500 kwa siku. Hii ni kwa sababu iwapo kiwango cha kalori
kitakuwa kidogo kuliko hitajio la mwili, ufanisi wa mwili hupungua na
kiwango cha misuli hupungua suala linaloweza kusababisha utapiamlo na
matatizo mengine ya kiafya.
&&&&&
Iliyopo hewani ni idhaa ya Kiswahili sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran na kipindi kilichopo hewani ni Ijuwe Afya Yako. Wasikilizaji
wapenzi kwa kuwa baadhi ya wasikilizaji wetu wametuandikia na kutaka
kujua namna ya kupunguza unene, tumeamua kuelezea moja ya njia za
kupunguza nene au diet plan. Kuna njia nyingi sana ambazo hutumiwa na
watu ili kupunguza mwili na tumbo, lakini baadhi huwa ngumu sana au
zinakuwa haziendani na mazingira wanayoishi watu, hivyo watu wengi
hushindwa njiani. Zipo njia za kutumia madawa kama kahawa, chai ya
kupunguza uzito na vinginevyo ambazo huwa si za kudumu na hata baadhi ya
wakati huwa na madhara. Lakini njia hii ifuatayo unaweza kuifanya ikawa
ni maisha yako ya kila siku ikazoeleka na ukawa unaishi hivyo hivyo
bila kuongezeka uzito wa mwili. Tutatoa mfano wa kupunguza uzito kwa
muda wa siku 7. Mambo muhimu ya kuzingatia ni kwamba, kupungua uzito
kunategemea kiwango cha mafuta mwilini (body fat), uzito wa mtu, kalori
anazohitaji kwa siku, BMI yake pamoja na lengo la mtu kutaka kupunguza
uzito. Maswali muhimu ya kujiiuliza ni kuwa, je, vyakula ninavyokula
hunipa nguvu na uwezo wa kumudu majukumu yangu ya kila siku? Nahitaji
kupunguza kiwango cha mafuta mwilini kwa kiasi gani? Kwa mfano wengine
wanahitaji kupunguza asilimia 10, 20 au 25 ya kiwango cha mafuta
mwilini. Kwa maana hiyo, si kila diet plan humfaa kila mtu, inaweza
ikawafaa baadhi na isiwafae wengine.Jambo lingine la kuzingatia ili kupungua uzito ni kufuata ushauri wa wataalamu wa lishe, madaktari, wataalamu wa mazoezi na kadhalika. Ufuatao ni mfano wa njia ya kupunguza unene au diet plan. Kila siku unahitaji kunywa kikombe kimoja cha kahawa, na ni vizuri kubadilisha unywaji wa kahawa kwa chai, yaani kama leo utakunywa kahawa kesho kunywa chai na kadhalika. Kwa wale wenye ugonjwa wa shinikizo la damu, ugonjwa wa wasiwasi na kadhalika, wanashauriwa kuepuka kahawa kabisa na hivyo wanywe chai. Wagonjwa wa kisukari wanaweza kunywa chai au kahawa kwa kukamulia ndimu au limao ndani yake na hivyo kuongeza ladha.
&&&&&
Siku ya kwanza:Tembea kwa muda wa dakika 30 asubuhi au jioni kabla ya kula chakula chochote. Kwa wale wenye mashine ya kutembelea ya tredmill wanaweza kutembea kwa muda wa dakika 30 kwa kuanza na kasi ndogo. Unaweza pia kukimbia kwa muda wa nusu saa au kukimbia kwenye mashine ya tredmill kwa muda wa nusu saa. Anza kukimbia kwa kasi ndogo halafu ongeza kasi. Au unaweza kukimbia kwa kasi ya juu kama 8 kwa muda wa dakika 5 na kisha kupunguza hadi 5. Hii inaitwa interval training, yenye lengo la kukupa uwezo wa kufikisha dakika 30, kuchoma mafuta mwilini na kupunguza mapigo ya moyo ili yarudi kwenye kiwango cha kawaida. Hii ni kwa sababu wakati unapofanya mazoezi mapigo ya moyo huongezeka sana na pia kuupa moyo wako uwezo wa kufanya kazi vizuri. Wale wenye matatizo ya kiafya ya mapigo ya moyo au wale ambao walishawahi kuugua hapo awali matatizo ya moyo na wagonjwa wa pumu, ni vyema wafanye mazoezi chini ya uangalizi wa wataalamu wa mazoezi pamoja na kushauriana na daktari. Fanya mazoezi ya tumbo (sit-ups) mara 15-20. Ikiona ni vigumu kwako unaweza kuanza hata kwa mara 10 na utakuwa unaongeza kadri siku zinavyoenda na kadri utavyokuwa unazoea maumivu ya nyama za mbavu na tumbo. Unaweza kutumia benchi au kulala sakafuni. Ukimaliza kutembea na kufanya sit-ups, kunywa maji ya uvuguvugu glasi 4. Siyo lazima unywe yote kwa wakati mmoja. Unaweza ukawa unakunywa huku ukiendelea na mambo mengine mpaka bilauri 4 ziishe. Ili kuongezea ladha unaweza kukamulia ndimu au limao katika maji hayo ya uvuguvugu. Limao na ndimu siyo tu huongeza ladha bali pia vinasaidia kupunguza mafuta mwilini.Mlo wa asubuhi (Breakfast):Kunywa kikombe kimoja cha kahawa au chai kwa kuweka kijiko kimoja kidogo cha sukari. Yai moja la kuchemsha na kipande kimoja cha mkate wa kawawia au ngano isiyokobolewa (brown bread). Usithubutu kuweka siagi wala kitu kingine chenye mafuta na sukari nyingi. Kula matunda kadri unavyoweza lakini epuka ndizi tamu.Chakula cha mchana (Lunch):Kula robo kuku wa kuchoma au wa kuchemsha na si vinginevyo. Saladiau kachumbari ya mboga mboga tofauti lakini isiwe na sosi ya mayonnaise. Kunywa maji ya uvuguvugu glasi 4 tena. Jitahidi kuepuka snacks au asusa kama vile malai (ice cream) chokoleti, biskuti na kadhalika. Jizoeshe kula matunda kwa wingi kila unapohisi njaa. Jioni tembea au kimbia tena kwa muda wa nusu saa pamoja na kufanya mazoezi ya sit-ups wakati unasubiri chakula cha usiku. Chakula cha usiku (Dinner):Kulasupu ya samaki yoyote yule bakuli kubwa la kutosha. Unaweza kutumia karoti, nyanya au tungule, brokoli,cauliflower, pilipili boga na za kuwasha, ndimu au limao, kitunguu maji na thomu na kadhalika epuka viazi vyovyote vile kwenye supu.
Naam wapenzi wasikilizaji tunaishia hapa kwa leo kwani muda wa kipindi chetu umetutupa mkono. Hadi wiki ijayo kwaherini.
No comments:
Post a Comment