Monday, May 27, 2013

VIKONGWE WATATU WAUAWA KIKATILI KWA KUCHOMWA MOTO HUKO BUNDA


MAUAJI ya kikatili yametokea usiku wa kuamkia leo wilayani Bunda, mkoani Mara baada ya watu wenye hasira wa kijiji cha Kasaula kuwauwa kwa kuwachinja kama Kuku kisha kuwachoma moto vikongwe watatu kwa kuwatuhumu wanajihusisha na vitendo vya kishirikina. 
 Pia watu hao mbali na kuwaua kikatili vikongwe hao kwa tuhuma kwamba walimuua kijana mmoja aitwaye Sale Ligolo, walichoma moto na kuteketeza nyumba walizokuwa wakiishi wazee hao pamoja na kupora kuku waliokuwa wakiwafuga na kuwatafuna kumaliza hasira zao.
 Kwa mujibu wa wa taarifa ya mwandishi Masau Bwire aliyepo Bunda kwa sasa, tukio hilo limetokea usiku wa kumakia leo baada ya watu hao wenye hasira kuwasaka ajuza hao baada ya kuwepo tuhuma kwamba walishirikiana kumuua kijana huyo hivi karibuni.
Kijana huyo alikufa kwa kugongwa na gari, lakini dereva aliyemgonga alidai hakuona kama alimgonga mtu ila mbwa na pia inaelezwa  tangu azikwe kijana huyo alikuwa akirejea kwa mkewe na kumuita nyakati za usiku pamoja na kusumbua familia yao akitaka apewe chakula na ndipo wanafamilia hao walipoamua kwenda kwa mganga kuchunguza tukio hilo. 
 Wakiwa kwa mganga,wanafamilia hao walitajiwa majina ya wanakijiji watatu wa kijiji hicho ambao hata hivyo walitoroka kwenda vijiji vya jirani pamoja na familia zao kabla ya usiku wa leo kuvamiwa walipokuwepo na kuangushiwa adhabu hizo za kinyama. 
Wa kwanza kushambuliwa na kuuwa ni bibi aitwaye Bi Mgala ambaye alikimbilia kijiji cha jiorani kwa rafiki yake aitwaye Bi Laya, ambapo walimkata miguu yote miwili na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili kabla ya kumchoma moto ambapo hata hivyo kitu cha ajabu ni kwamba ziliungua nguo zake tu huku mwili ukiwa upo vile vile. 
Baadaye walimgeukia Bi Laya aliyekuwa akitaka kuwatoroka na kumfanyia unyama kama rafikie kwa kosa la kumhifadhi Bi Mgala kwa kuamini huenda wanafanya shughuli za kishirikina pamoja na baadaye kurudi Kasaula na kumnasa Bi Chausiku na kumfanyia kama walivyowafanyia ajuza hao wengine kisha kuchoma nyumba tatu. 
 Bibi wa tatu wanayemtuhumu pia kwa ushirikina, ametimka kijijini hapo, lakini nyumba yake imeteketezwa pamoja na kuku waliokuwa wakiwafuga kuporwa na watu hao na kutumia moto waliouwasha katika nyumba hizo kuwachoma na kuwala kwa hasira. 
Kamanda wa Polisi wa Bunda, Mika David Nyange amethibitisha juu ya tukio hilo la kusikitisha na kwamba wanedelea na upelelezi kwa nia ya kuwasaka waliohusika na kitendo hicho cha kujichukulia sheria mikononi.

No comments: