Saturday, December 29, 2012

KESI YA LWAKATARE: TUNDU LISU AMLAUMU "ISSA MICHUZI" NA " MWIGULU NCHEMBA"



Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki  (CHADEMA), Tundu Lissu akiongea na wanahabari (hawapo pichani).
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu leo amefanya mkutano wa wanahabari. Katika mkutano huo, Lissu ameongea yafuatayo:

1. Atafungua kesi Mahakama kuu kuiomba iiamuru Mahakama ya Kisutu kuendelea kusikiliza kesi ya awali iliyofutwa na DPP katika kesi inayomhusu Lwakatare kwani DPP amevuka mipaka yake inayomruhusu kufuta kesi na isitoshe kesi aliyofungua ni ile ile hivyo Mahakama iamuru shauri la awali liendelee.


2. Kuhusu video iliyoonyeshwa kwenye mitandao Lissu anasema kuna mashaka makubwa sana kuhusiana na video ile na kisheria kesi hiyo ikifika mahakamani haitachukua hata nusu saa ataibuka mshindi.
Lissu anasema
- Hakuna mtu anayepanga mauaji katika hadhara mahali ambapo watu wanapitapita kama inavyoonekana kwenye video ile.


-Lwakatare kama alirekodiwa basi lazima ielezwe je ilikuwa ni kwa hiari yake kama si hivyo ni makosa


-Issa Michuzi Mpiga picha wa Rais alikuwa akipongezana na watu wa Ikulu wenzake kuwa TISS (Usalama wa Taifa) wamefanya kazi nzuri kwa kurekodi ile video. Kisheria usalama wa taifa hawatakiwi wala hawaruhusiwi kurekodi au kuvifanyia ushushu vyama vya siasa kwa maslahi ya Chama tawala.


-Ludovick baada ya kukutana na Lwakatale tarehe 28 Desemba mwaka jana saa 5 muda mfupi baadaye yaani saa 5:59 alimpigia simu Mwigulu Nchemba kwa kutumia namba ya simu ya Mwigulu ambayo ameiandikisha kwenye kumbukumbu na vitabu vya Bunge Lissu anadai wana rekodi ya mazungumzo yao.


-Siku iliyofuata tarehe 29 Desemba mwaka jana akiwa kwenye kipindi cha Tuongee asubuhi cha Star TV alidai ana mkanda wa video unaowaonyesha CHADEMA wakipanga mauaji.


-Pia amedai itabidi waambiwe video hiyo imerekodiwa studio gani, maneno gani yameondolewa na yapi yameongezwa.


Anamalizia kwa kusema walianza kwa kusema CHADEMA ni chama cha familia wakashindwa, wakasema ni chama cha wachaga wakashindwa, wakesema ni chama cha wakatoliki wakashindwa, wakasema ni chama cha wakristo wakashindwa, wakasema ni chama cha ukanda wakashindwa leo wanasema ni chama cha kigaidi WATASHINDWA.


(Picha / Habari na Kurugenzi Ya Habari Chadema)

MAELFU WAANDAMANA KUPINGA GESI KUTOLEWA MTWARA


MAELFU ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara jana waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka hapa kwenda Dar es Salaam.


Maandamano hayo ambayo yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huu zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.

Waandamanaji hao waliotembea umbali wa kilomita sita, walitoa maazimio tisa mojawapo likihoji sababu za mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na inakochimbwa gesi hiyo.

Katika tamko hilo lenye kurasa mbili, waandamanaji hao wamesema Serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo, huku tayari Rais Jakaya Kikwete akiwa ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam. Wametaka ujenzi huo usitishwe.

Pia wamesema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani hapa mwaka 2009 kwamba ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.

Aidha, wanataka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.

“Tunahitaji viwanda vikubwa vijengwe Mtwara ili kuleta ajira kwa wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani, tuna hofu kutokana na ilivyokuwa kwa wakazi wa Songongo (Lindi) kubaki maskini wakati gesi inazalishwa hapo, yasije yakatukuta sisi, hivyo ni lazima tusimamie rasilimali hii ili iweze kuleta maendeleo,” walisema katika azimio lao.

Wamesema pia kwamba Serikali haijaeleza athari zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa gesi katika eneo hilo na namna itakavyoweza kusaidia kuziondoa, huku wakitaka gharama za uunganishaji wa umeme wa nyumbani zisizidi Sh50,000 ili kila mwananchi aone ananufaika na gesi hiyo.

Waandamanaji hao wamesema gharama za mradi huo wa kusafirisha gesi hadi Dar sa Salaam ni kubwa, hivyo wakashauri Serikali ichimbe gesi ya Dar es Salaam katika kisima namba 7 ili kuepuka hasara.

Katika azimio lao la mwisho, wamemwomba Rais Kikwete kumwondoa madarakani Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia kwa madai kwamba amewakashifu kutokana na madai yao ya kupinga gesi kwenda Dar es Salaam.

Ilielezwa kuwa, awali Simbakalia aliombwa kuwa mgeni rasmi katika maandamano hayo, lakini alikataa na badala yake yalipokewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Siasa, Hussein Mussa Amiri.

Desemba 21, mwaka huu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara (RCC), kilichoketi kwenye Ukumbi wa Boma, Simbakalia alisema hawezi kushiriki katika maandamano hayo.

Maandamano hayo yaliratibiwa na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, yakiwa na kaulimbiu ya ‘gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.’ Kutokana na maandamano hayo, Soko Kuu la Mtwara lilifungwa kwa muda kutoa fursa kwa wafanyabiashara hao kushiriki na barabara kadhaa zilifungwa kwa muda.

Mbali ya watu kujitokeza kwa wingi, pia walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.

“Bandari Bagamoyo, Viwanda Bagamoyo, Gesi Bagamoyo, Mtwara wapuuzi?.... Gesi haitoki hata kama hatujasoma.... Gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.... Kusini tumedharauliwa vya kutosha sasa basi.”

Akisoma tamko la vyama hivyo, Katibu wa umoja huo, Seleman Litope alisema kwa muda mrefu Kusini imekuwa ikiondolewa fursa mbalimbali za maendeleo.

Alitoa mfano wa kung’olewa kwa reli, ukosefu wa usimamizi mzuri wa zao la korosho, ukosefu wa miundombinu ya barabara, kuondolewa kwa Mradi wa Maendeleo ya Ukanda wa Mtwara (Mtwara coridor) na hilo la gesi.

Alisema hali hiyo imesababisha mikoa ya Kusini kuwa nyuma kimaendeleo na kwamba umoja wao unalenga kuhakikisha rasilimali yao hiyo haitoki kwenda kokote kabla ya kuwanufaisha.

No comments: