Wednesday, January 30, 2013

BUNGE LAUNDA KAMATI MAALUMU KWENDA MTWARA


Spika wa Bunge bi Anne Makinda amesema Bunge limeunda Kamati Maalumu kwenda mkoani Mtwara kutafuta suluhu kuhusu suala la nishati ya gesi, iliyopatikana mkoani humo.

Spika Makinda ameyasema hayo wakati akiahirisha kikao cha Bunge kilichoanza leo Mkoani Dodoma.

Spika amesema matokeo ya Kamati hiyo Maalumu yatawasilishwa kujadiliwa Bungeni.

Iddi Maalim wa TBC anaripoti katika taarifa iliyosomwa saa saba mchana ifuatavyo:

Bunge sasa linaunda Kamati ambayo itakwenda Mtwara, kuwasikiliza Wananchi halafu ndani ya kikao hiki –mkutano huu unaofanyika– Kamati ya Bunge itakuwa imekwenda Mtwara, itawasikiliza Wananchi, italeta masuala ambayo yanazungumzwa kule Mtwara kisha yatajadiliwa.

Hili alikuwa analizungumza baada ya kusema kuwa amepokea vikaratasi na maombi mengi kwamba Bunge lijadili suala la Mtwara, gesi kama suala ambalo ni la dharura.

Lakini akasema kwamba, ile hoja si ya dharura na akaeleza pia ukweli kwamba Wabunge ambao wanasema lijadiliwe kama suala la dharura wengi wao hawalifahamu kwa undani, kwa hiyo badala ya kujadili jambo ambalo hawalifahamu kwa undani, ni afadhali ataunda kamati ambayo itakwenda Mtwara ikirudi itakuja na majibu, na mapendekezo ya Wananchi na ndipo Bunge litajadili ndani ya Mkutano huu wa kumi.

No comments: