FUNDI magari, David Kweka, mkazi wa Manzese Tip Top jijini Dar es
Salaam, amepigwa risasi na kujeruhiwa mkono wake wa kulia baada ya
kutokea ubishi wakati alipokuwa akiangalia mechi ya kombe la FA kati ya
Manchester United na Chelsea Jumapili iliyopita.
Tukio hilo la aina yake, limetokea katika baa ya Dolphin, Sinza
Kumekucha jijini Dar baada ya shabiki mmoja wa Man United kuchomoa
bastola na kuzua kizaazaa hicho.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio
hilo, David alifika Sinza akiambatana na kaka yake, Elnadia Kweka kwa
ajili ya kuangalia mechi hiyo iliyokuwa inaoneshwa katika runinga ya baa
hiyo na wote walikuwa wakishabikia klabu ya Chelsea.
Wakati Man
United ikiwa inaongoza mabao 2-0, mashabiki wa timu hiyo walikuwa
wakitamba na kutoa maneno ya kejeli kuonesha kwamba wao ndiyo wababe wa
soka nchini England.
David na kaka yake hawakuwa na la kusema hadi Chelsea iliposawazisha mabao hayo na ubao wa matokeo kusomeka 2-2.
Pamoja na hali hiyo, mashabiki wa Man United waliendeleza tambo kwa
kudai kwamba lazima watapata bao la tatu wakati wowote na kumaliza
mchezo huo wakiwa washindi.
Wakati tambo hizo zikiendelea, Elnadia alishikwa na haja ndogo na kutaka
kwenda msalani, ndipo mtu aliyejulikana kwa jina moja la Wambura
aliyekuwa akishabikia Man United alipomzuia na kumwambia kuwa alikuwa
akitaka kukimbia.
“Ulitokea ubishi mkubwa kati ya Elnadia na Wambura
ambaye alijitambulisha kama afisa usalama na ulipozidi, shabiki huyo wa
Man United alichomoa bastola na kumtishia.
“Hali hiyo ilizua
kizaazaa ndipo David alipoamua kumvaa Wambura na kutaka kumnyang’anya
bastola yake ili kumuokoa kaka yake. Wawili hao walinyang’anyana bastola
hiyo kwa muda mrefu hadi ilipofyatuka risasi tatu kwa bahati mbaya,”
alisema shuhuda mmoja.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, risasi moja kati ya hizo ilimpata David katika mkono wake wa kulia.
Watu walitawanyika na baada ya muda David alichukuliwa na kupelekwa
Hospitali ya Palestina ambako alishonwa nyuzi 12 katika mkono wake.
Taarifa zaidi za tukio hilo zinasema kuwa David alipoteza shilingi
milioni moja la laki saba ambazo alipewa na mteja wake kwa ajili ya
kwenda kumnunulia ‘gear box’.
Habari zaidi zinasema, jalada la kesi
hiyo limefunguliwa katika Kituo cha Polisi cha Urafiki, Ubungo jijini
Dar kwa namba URP/RB 17878/2013, KUJERUHI KWA SILAHA.
Kwa mujibu wa
askari mmoja wa kituo hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini
kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo, Wambura anashikiliwa katika kituo
hicho.
No comments:
Post a Comment