Na Anna Nkinda – Maelezo, Mwanza
Imeelezwa
kuwa kutokana na tatizo la baadhi ya kina mama wajawazito kuchelewa
kufika Hospitali mapema kujifungua wengi wao wanakufa kutokana na tatizo
la kupasuka kwa mfuko wa uzazi, kutokwa na damu nyingi kabla na baada
ya kujifungua na kifafa cha mimba.
Hayo
yamesemwa jana na Daktari wa Mkoa wa Mwanza Dk. Valentino Bangi wakati
akisoma taarifa ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza - Sekou Toure
kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyefika Hospitalini hapo kwa ajili
ya kufungua mradi wa kisima cha maji uliojengwa na Kampuni ya bia ya
Serengeti.
Dk.
Bangi alisema kuwa tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto
limepungua kwa kiasi kikubwa katika Hospitali hiyo ukilinganisha na
miaka ya nyuma kwani mwaka 2012 vifo vilivyotokana na tatizo la uzazi
vilikuwa 10 ukilinganisha na mwaka 2011 ambapo kulikuwa na vifo 15.
“Kiwango
cha utoaji wa chanjo kwa watoto kimeongezeka katika mkoa wetu na
kufikia asilimia 95, jumla ya watoto 91194 ambao ni sawa na asilimia 85
waliolazwa walipata chanjo ya pepopunda na vifo vya watoto chini ya
mwaka mmoja ni vimepungua na kufikia 11 kati ya vizazi hai 1000”,
alisema Dk. Bangi.
Aliendelea
kusema kuwa wamefanikiwa kukarabati jengo la upasuaji, wodi ya watoto,
wagonjwa mahututi wodi ya kujifungua kina mama, kuajiri watumishi wa
kada mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa watano, ujenzi wa vyumba vya
kuhifadhia chanjo, jengo la wagonjwa wa afya ya akili, na maabara ya
kisasa kupitia msaada wa watu wa Marekani.
Dk.
Bangi alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa
dawa, vifaa tiba na watumishi wenye ujuzi, bajeti finyu katika
uendeshaji wa huduma za afya, uchakavu wa majengo, kukosa mfumo imara wa
rufaa kuanzia zahanati hadi hospitali ya rufaa, ukosefu wa nyumba za
watumishi, kushindwa kukamilisha jengo la upasuajai la akina mama
wajawazito na kuongezeka kwa makundi mbalimbali ya misamaha katika kutoa
huduma za afya.
Kwa
upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake
na Maendeleo (WAMA) aliishukuru kampuni ya bia ya Serengeti kwa kujenga
mradi wa kisima cha maji ambacho kitapunguza tatizo la maji katika
Hospitali hiyo na kusema kuwa kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kutoa
michango ya maendeleo na hasa kusaidia miradi ya upatikanaji wa maji
safi na salama kwa jamii ambayo imeonyesha tija na kuboresha maisha ya
watanzani kwa kujenga jamii yenye afya bora kwa maendeleo kwa taifa.
Mama
Kikwete alisema, “Maji ni nguzo kubwa kwa maendeleo katika nyanja zote
za kiuchumi na kijamii mahali popote pale Duniani , hakika kukamilika
kwa mradi huu ni hatua muhimu sana ya kuboresha huduma za maji katika
hospitali zetu hapa nchini, ambazo zinahitaji huduma ya uhakika ya maji
safi na salama ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya wagonjwa pamoja na ya
watoa huduma”.
Alimalizia
kwa kutoa wito kwa uongozi wa Hospitali hiyo kuulinda mradi wa maji ili
kuufanya uwe endelevu, kwa kufanya hivyo mradi huo utakuwa umetoa
mchango mkubwa katika kuendeleza ufanisi wa huduma kwa wagonjwa na
wataalamu wa afya.
Akisoma
taarifa ya mradi huo Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya
bia ya Serengeti Jaji Mark Bomani alisema kuwa mradi wa maji umegharimu
zaidi ya shilingi milioni 70 na una kisima kinachoweza kutoa lita 240000
za maji kwa siku, pampu ya maji ya umeme na tanki la lita 10000.
“Kampuni
yetu kupitia mpango wake wa kuisaidia jamii na mpango rasmi wa kusaidia
upatikanaji wa maji safi na salama leo imefikia lengo la kusaidia watu
zaidi ya 160000 wanaohudumiwa na Hospitali hii, hakika mradi huu
utachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa ya mlipuko na vifo vya
kina mama wajawazito na watoto”, Jali Bomani alisema.
Alisema
kuwa kwa kutambua umuhimu wa kuisaidia jamii na siyo tu kupitia miradi
ya maendeleo bali pia kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakuwa endelevu na
kuleta tija kwa jamii husika. Kampuni hiyo pia wanaisaidia jamii katika
upande wa afya, mazingira na kutoa ufadhili wa masomo wa elimu ya juu
kwa wanafunzi ambao wamefanya vizuri lakini hawana uwezo wa kumudu
gharama za masomo.
Licha
ya kujenga maradi wa kisima cha maji katika hospitli hiyo, kampuni hiyo
pia imeshafadhili miradi mingine ya maji ambayo imewafikia watu 350000
katika Hositali za Frelimo-Iringa, Temeke – Dar –es-Salaam , Mawenzi –
Moshi na mradi wa maji wa mkuranga ambao unawahudumia watu zaidi ya
250000.
No comments:
Post a Comment