Friday, January 11, 2013

Default Mwigulu Nchemba: CHADEMA itakufa 2015


Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba

CHAMA Cha Mapinduzi kimekitabiria kifo Chadema baada ya uchaguzi wa 2015 kikieleza kuwa CCM ikishinda, chama hicho kitakuwa hakina nguvu tena kwa kuwa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa atakuwa amechoka.


Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba aliliambia gazeti hili jana kuwa chama hicho kinapoteza umaarufu kadri siku zinavyokwenda hasa kutokana na siasa zake za uchochezi na mwaka 2015 ndio itakuwa mwisho wa chama hicho.


Alisema kitakufa na kitasahaulika kabisa, akisema sasa hivi vijana wameshaanza kuwakimbia, na kwamba anaamini pia baada ya 2015 hakuna diwani ambaye atagombea kupitia chama hicho.


Alisema pia ni mwaka ambao Katibu wa Chadema Willibrod Slaa amestaafu kwa kuwa alishatangaza asiposhinda atastaafu na Chadema haiwezi kushinda hivyo mwisho wa Dk Slaa ndio utakuwa umefika kwa kuwa nyota yake haitang’aa tena.


“Nguvu ya Dk Slaa aliyokuwa nayo miaka miwili iliyopita sio aliyonayo sasa na mpaka mwaka 2015 atakuwa ameisha kabisa.” alisisitiza.


Pia Mwigulu aliyataka makundi yaliyojichomoza ndani ya CCM ikiwa ni harakati za kuwania urais mwaka 2015 kuheshimu ilani ya chama hicho kwa kuitekeleza na kuisimamia kwa kutoleta vurugu ndani ya chama wala kujenga chuki kwa wale ambao hawawaungi mkono.


|”CCM ina utaratibu wake wa kupata mgombea na hatumzuii mtu kugombea, sisi kama kamati ya utendaji tunatekeleza maagizo aliyotoa mwenyekiti tutayasimamia kwa nguvu zote anayetaka kugombea ahakikishe havurugi chama na asitengeneze chuki kwa ambao hawamuungi mkono.”


Wakati huohuo Naibu Katibu huyo wa CCM na Mbunge wa Iramba Mashariki aliwataka wakazi wa Mtwara kuachana na propaganda zinazoenezwa na wapinzani kuhusu rasilimali ya gesi na badala yake wafanye kazi kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.


“Rasilimali iliyopo ni ya taifa na watafaidika, hakuna rasilimali ya wilaya fulani, bomba la gesi ni lazima lijengwe tutawaelimisha wakazi wa Mtwara, kwani hata Ziwa Victoria bomba lilijengwa kwenda Shinyanga badala ya Kwimba, kwa nini basi halikujengwa kwenda Kwimba wakati pale ni karibu zaidi.


“Utajiri unategemea na jitihada, wasitegemee kwa vile tuna rasilimali ya gesi basi wakae wategemee watapata utajiri bila ya kufanya kazi haiwezekani, wasisubiri kupewa vya bure, ni kama mikoa yenye madini halafu wakazi wa pale wategemee Serikali itawapa vocha za kuweka kwenye simu kwa vile madini yao kwao, haiwezekani ni lazima wafanye kazi.

Source: Mwananchi

No comments: