Sunday, September 29, 2013

SERIKALI YAYAFUNGIA MAGAZETI YA MWANANCHI NA MTANZANIA KWA UCHOCHEZI

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeyafunga magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai kuwa  yanaandika habari za uchochezi na uhasama.

Imeelezwa kuwa kutokana na habari ambazo zinachapishwa na magazeti hayo zinasababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hivyo kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), ni kwamba Gazeti la Mwananchi limefungiwa kutochapishwa kwa siku 14,  kuanzia Septemba 27, 2013.

"Adhabu hii imetangazwa kwa tangazo la Serikali namba 333 la Septemba 27, 2013.
Gazeti la Mwananchi limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani.

"Mfano Julai 17, 2013 katika toleo namba 4774 ilichapisha habari isemayo "MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013" kwa kuchapisha waraka uliozuiwa kwa matumizi ya vyombo vya habari. Waraka huo ulikuwa wa siri kwani haukupaswa kuchapishwa magazetini," ilisema taarifa hiyo.

Aidha, katika toleo la Agosti 17, 2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho "Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali" habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira.

"Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri  kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu. Jambo ambalo halikuwa la  ukweli," ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Jeshi la Polisi katika doria yake siku hiyo halikupeleka mbwa katika maeneo ya misikiti na kwamba Serikali na Jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu.

Kwa mazingira hayo, taarifa hiyo ilisema jeshi haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada, hivyo gazeti hilo kuchapisha habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya Kiislamu kwani mbwa ni najisi kwa sababu hapaswi kuingia katika maeneo ya ibada.

Wakati Gazeti la Mtanzania limefungiwa kutochapishwa kwa siku 90, kuanzia Septemba 27, 2013 kwa kuchapisha habari zenye uchochezi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Serikali ni kwamba gazeti hilo limeonywa mara nyingi lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili na sheria na kanuni za fani ya habari.

Pamoja na kuonywa gazeti hilo halikuonesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti kwani katika toleo namba 7262 la Machi 20, 2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho "URAIS WA DAMU".

Pia Juni 12,  2013, toleo namba 7344 lilichapisha makala isemayo "mapinduzi hayaepukiki". Aidha, Septemba18, 2013 katika toleo namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha kichwa cha habari kisemacho "Serikali yanuka damu".

Serikali ilisema taarifa hiyo ilikolezwa na picha zilizounganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika .

"Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga waliumizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliovamiwa na kujeruhiwa vibaya.

"Vile vile gazeti hilo limeishtumu Serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi. Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama wavione kuwa haviwasaidii.

"Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu Serikali imelifungia Gazeti la Mtanzania  kutochapishwa kwa muda wa siku 90 kwa tangazo la Serikali namba 332 la  Septemba 27, 2013," ilisema taarifa hiyo.

Pia ilifafanua kuwa Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini, kuzingatia weledi, miiko na madili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Serikali inawataka wamiliki na hasa wahariri kuhakikisha habari wanazoandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia taaluma, kuweka mbele maslahi ya taifa na uzalendo wa hali ya juu.

Pia inavionya vyombo vya habari vinavyotumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo kuvifungia. Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari vikiwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini.

No comments: