Tuesday, April 30, 2013

MAELEZO KUHUSU HALMASHAURI YA WILAYA YA MULEBA



 
Wilaya ya Muleba ni mojawapo ya Wilaya saba zinazounda Mkoa wa Kagera. Wilaya hii ipo kati ya longitude 31 o 30' na 32 o 5' Mashariki ya Griniwich na Latitude 1 o 30' na 2 o 20' Kusini ya Ikweta.
Kabla ya mwaka 1975 Wilaya ya Muleba ilikuwa ni Tarafa mojawapo ya Wilaya ya Bukoba. Mwaka 1975 tarafa ya Muleba ilipewa hadhi ya kuwa Wilaya na makao yake makuu yalikuwa Kaigara. Mwaka 1977 majengo ya uhakika ya ofisi yalijengwa Kibonwangoma – eneo ambao lilikuwa ni maarufu kimila kwa shughuli za watemi (Bakama) na utawala wa Wilaya ulihamia huko. Shughuli za Halmashauri hata hivyo hazikuanza mara moja hadi mwaka 1984.
 
 
 
Wilaya inapakana na Wilaya ya Bukoba upande wa Kaskazini, Magharibi inapakana na Wilaya ya Karagwe, Kusini inapaka na Wilaya ya Biharamulo, Kusini Mashariki inapakana na Wilaya ya Chato na Mashariki inapakana na Mkoa wa Mwanza.
Wilaya ina eneo la kilomita za mraba 10,739 na kati ya hizo kilomita za mraba 3,444 ni nchi kavu na kilomita za mraba 7,295 ni eneo la maji hususani Ziwa Victoria . Eneo la nchi kavu linahusisha pia zaidi ya visiwa ishirini vilivyomo katika Ziwa Victoria .
JIOGRAFIA YA WILAYA
Wilaya ya Muleba imetawaliwa na vilima, mabonde na tambarale (plateaus). Wilaya ipo kati ya mwinuko wa mita 1,150 na 1,667 kutoka usawa wa bahari na sehemu ya juu kabisa ni Karambi. Mto Ngono unakatisha wilaya kuanzia Kusini kuelekea Kaskazini ambapo unaungana na Mto Kagera unaomwaga maji yake katika Ziwa Victoria.
Wilaya imegawanyika katika kanda kuu nne za kilimo ambazo ni: Ukanda wa mwambao wa Ziwa na Visiwa katika Ziwa Victoria, Ukanda wa juu, Ukanda wa chini Kusini na Ukanda wa Burigi. Ukanda wa mwambao wa Ziwa na ukanda wa juu unapata kipindi kirefu cha unyevunyevu (miezi 8 – 9) wakati ukanda wa chini na wa Burigi unapata kipindi cha unyevunyevu cha miezi 3 – 4 tu kwa mwaka.
Mvua zinanyesha zaidi upande wa Kaskazini – Mashariki yaani milimita 1800 wakati Kusini – Magharibi ni pakame. Kwa kufuata viwango vya miinuko na mvua, Wilaya inakuwa na kanda za kilimo tofauti zenye mazao mbali mbali yanayopandwa katika misimu tofauti.
Hali ya rutuba ya udongo si ya kuridhisha hasa kutokana na mvua nyingi zinazosababisha kuondolewa kwa virutubisho udongoni. Hata hivyo maeneo ya mabonde ya upande wa Kusini – Magharibi na miinuko tambarale (plateaus) yana rutuba ya kutosha wakati maeneo ya mwambao wa ziwa hayana rutuba.
IDADI YA WATU
Kulingana na takwimu za sensa ya watu na makazi za mwaka 2002 na ongezeko la watu la asilimia 2.5 kwa mwaka wilaya kufikia mwaka huu wa 2008 inakadiriwa kuwa na jumla ya watu wapatao 453,931 na kati ya hao watu 225,891 ni wanaume na watu 228,039 ni wanawake.
Msongamano wa watu kwa kilomita ya mraba ni 110. Watu wenye uwezo wa kufanya kazi ni asilimia 24 ya watu wote wakati watu wenye umri wa kwenda shule ni asilimia 30, zipo kaya 81,084 na wastani wa watu katika kaya ni 4.7.
Jedwali Na.1, 2 na 3 hapa chini vinachambua kwa kina takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 kama ifuatavyo:-
Jedwali Na. 1 : Idadi ya watu kwa umri na jinsi
Umri
Me
Ke
Jumla
0 -1
29718
32219
61937
1 – 5
29860
30760
60620
6 – 14
31518
28519
60037
15 – 24
34951
33697
68648
25 – 44
29331
25584
54915
45 – 60
19971
22957
42928
60+
16903
20340
37243
Jedwali Na. 3: Mlinganisho wa jinsi katika Grafu
Jedwali Na. 3: Idadi ya watu Kitarafa.
Tarafa
Idadi ya Kata
Idadi
ya vijiji
Idadi ya Mitaa
Me
Ke
Jumla
Muleba
6
22
2
27354
27760
55114
Izigo
6
25
 
9123
8893
18016
Kamachumu
4
15
 
29988
30759
68648
Nshamba
9
39
 
72769
73398
146167
Kimwani
6
31
 
53018
53266
106284
Total
31
132
2
192252
194076
386328
 
UTAWALA NA UONGOZI KISIASA
KIUTAWALA
Kama ilivyoonyeshwa kwenye jedwali Na. hapo juu wilaya ya Muleba imegawanyika katika Tarafa tano (5) nazo ni Izigo, Kamachumu, Muleba, Nshamba na Kimwani. Tarafa hizo tano nazo zimegawanyika katika kata 31, vijiji 132, mitaa 2 na vitongoji 677.
KISIASA
Wilaya pia imegawanyika katika majimbo mawili ya uchaguzi. Jimbo la Muleba Kusini linaongozwa na Mh. Anna Tibaijuka (Mb) na Jimbo la Muleba Kaskazini linaongozwa na Mh. Mwijage (MB), na wote wawili wanatoka Chama Tawala cha CCM.
Upande wa Kata, Kata zote 30 zinao madiwani wa kuchaguliwa ambapo kata moja iko wazi baada ya diwani wake kufariki dunia na Kata 2 madiwani wake ni wa kutoka kambi ya upinzani. Madiwani hawa wote ni wanaume. Wapo pia madiwani 11 wanawake wa viti maalum ambapo 8 ni wa kutoka chama cha CCM na 3 wanatoka kwenye vyama vya TLP 1 na CUF 2.
 

UCHUMI
Pato la mwananchi wa Muleba linakadiriwa kuwa kati ya Tshs. 100,000 – 150,000 kwa mwaka. Hali hii ni chini ya mstari wa umaskini hivyo kuashiria kuwa wilaya hii ni kati ya wilaya maskini sana katika nchi ya Tanzania .
Zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Muleba wanategemea zaidi shughuli za kilimo kwa maisha yao ya kila siku. Zao kuu la biashara ni kahawa na mazao ya chakula ni ndizi na maharage. Kuporomoka kwa bei ya kahawa kumewakatisha tamaa wakulima hivyo kupelekea kutothanimi zao hili.
Zao la ndizi pamoja na kuwa ni zao la chakula pia huwapatia wakulima kipato kwani huuzwa katika masoko ya nje ya wilaya na mikoa jirani kama Mwanza na Shinyanga. Pia zao hili huwapatia wakulima kipato wanapotengeneza pombe ya kienyeji (Rubisi). Maharage mara nyingi hutumiwa na familia wakati zao la chai halipewi kipaumbele baada ya bei yake kuwa ya chini sana hivyo kupelekea wakulima kutelekeza mashamba.
 
           
           
 

No comments: